Walichozungumza Rais Magufuli na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki Baada Ya Kukutana Leo Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Novemba, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini na Mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu lililoundwa na Umoja wa Afrika (AU) kushughulikia tatizo la utoroshaji wa fedha (ikiwemo utakatishaji, wizi, rushwa na biashara haramu) kutoka Afrika Mhe. Thabo Mbeki, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mbeki amesema mazungumzo hayo yamemwezesha kupata taarifa na uzoefu muhimu kutoka kwa Mhe. Rais Magufuli kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kukabiliana na utoroshaji wa fedha katika maeneo mbalimbali yakiwemo sekta ya madini na rushwa, matatizo ambayo yanazikabili nchi zingine za Afrika.
“Ni wazi kwamba juhudi zinazofanywa na Tanzania zina umuhimu mkubwa kufanywa na nchi zingine za Afrika, kwa pamoja Waafrika tunaweza kukabiliana na utoroshaji wa fedha zetu kwenda nje ya nchi zetu, na Mhe. Rais Magufuli amezungumza kwa usahihi kabisa juu ya Matrilioni ya Dola za Marekani zinazopotea kupitia utoroshaji huo” amesisitiza Mhe. Mbeki.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Mstaafu Mbeki kwa kuongoza jopo hilo na kubainisha kuwa Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano utakaowezesha kunusuru rasilimali za Afrika, hivyo amemshauri kutenga muda wa kutosha ili apate taarifa za uhakika kutoka kwa viongozi na wataalamu katika mamlaka zinazodhibiti utoroshaji wa fedha hapa nchini.
Ripoti ya taasisi ya kimataifa iitwayo Global Financial Intergrity (GFI) ya mwaka 2014 kuhusu tatizo la utoroshaji wa fedha za Afrika inasema Afrika inapoteza Dola za Marekani kati ya Trilioni 1.4 na Trilioni 2.5 kwa mwaka kutokana na tatizo hilo, na kwamba kwa ujumla Afrika imepoteza Dola za Marekani Trilioni 95 kwa miaka 50 iliyopita, ikiwemo Tanzania iliyoripotiwa kupoteza dola za Marekani Bilioni 19 katika miaka 40 iliyopita.
“Na njia nyingi zinazotumika katika kutupotezea hizo fedha na kuibiwa, wanaweza wakaja kuwekeza lakini kila siku wakawa wanasema wanapata hasara kumbe hawapati hasara, wanatengeneza faida kubwa lakini kwenye vitabu wanawaandikia wanapata hasara, wanaweza wakaja kama wawekezaji na wakawa wanazidisha gharama za uwekezaji kuliko uhalisia” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Mhe. Nicolai Astrup, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumshukuru kwa mchango mkubwa ambao Norway inautoa katika maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali zikiwemo elimu, kilimo, nishati na gesi.
Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Mhe. Nicolai Astrup kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Norway ikiwemo kushirikiana na kampuni ya Equinor ya Norway katika uwekezaji wa kiwanda cha kusindika gesi asilia (LNG) kwa manufaa ya pande zote mbili, na kushirikiana na kampuni ya Yara ya Norway katika kuwawezesha wakulima kupata mbolea bora na gharama nafuu.
Nae Mhe. Nicolai Astrup amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupambana na rushwa, kuongeza ukusanyaji wa kodi na kuimarisha uchumi, na kwamba Norway itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mhe. Nicolai Astrup amebainisha kuwa pamoja na kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo umeme vijijini (REA) na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Norway itatoa Dola za Marekani Milioni 56 (sawa na shilingi Bilioni 127) kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba na Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Elisabeth Jacobsen.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Novemba, 2018
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment