Viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema na vyama rafiki wamefurika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kusikiliza rufaa ya dhamana ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Ester Matiko.
Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai na Matiko ambaye pia mweka hazina wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) wamekata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo baada ya kupatikana na kosa la kukiuka masharti ya dhamana waliyopewa awali.
Walifutiwa dhamana hiyo Novemba 23 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kufuatia maombi ya upande wa mashtaka kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana kwa kutokufika mahakamani tarehe ambazo kesi yao ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Mbowe na Matiko ambao wako mahabusu katika Gereza la Segerea walifikishwa mahakamani hapa mapema leo asubuhi
Miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa waliofika mahakamani hapo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika, wabunge na madiwani.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment