THRDC wamtaka Rais Magufuli ateue viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC), umemwandikia Rais John Magufuli waraka maalumu wa kumtaka kuteua viongozi katika ngazi mbalimbali ikiwamo Mwenyekiti, makamishna na makamishna wasaidizi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambao wamemaliza muda wao januari mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 28, Mratibu wa kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema tangu Januari mwaka huu hadi sasa viongozi hao muhimu hawako ofisini.

“Kwa mujibu wa Katiba ya nchi 1977 na sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya mwaka 2001, uwepo wa tume hiyo unajumlisha muundo wa uongozi ambao kwa sasa wamemaliza muda wake na ofisi kubaki bila watendaji hao,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, Wakili wa Mtandao huo, Deogratius Bwire, alizungumzia hali ya kifedha kuwa si nzuri kutokana na matumizi ya tume hiyo.

“Katika bajeti ya mwaka 2016/17 ilikuwa ni Sh 1.17, kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na miaka iliyopita na mahitaji ya tume hiyo,” alisema Bwire.


from MPEKUZI

Comments