Tanzania Kujenga Bandari Na Meli Za Uvuvi

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, amesema serikali ipo katika hatua nzuri ya kukamilisha hatua za ujenzi wa bandari ya uvuvi na kununua meli kwa ajili ya kuvua samaki kwenye eneo la bahari kuu pamoja na kuziwezesha meli nyingine kutia nanga katika bandari hiyo ikiwa ni lengo la Tanzania kwenda sambamba na nchi nyingine duniani kukuza uchumi kupitia sekta ya uvuvi.

Mhe. Ulega amebainisha hayo mara baada ya kuwasili nchini akitokea Mjini Nairobi nchini Kenya, ambapo hivi karibuni amehudhuria mkutano uliowajumuisha wajumbe zaidi ya elfu nne, kutoka mataifa mbalimbali, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewakilishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindudi Dkt. Ali Mohamed Shein.

Mhe. Ulega amesema mchango wa sekta ya uvuvi hapa nchini bado ni mdogo hivyo mkutano huo umeongeza hamasa kwa Tanzania kutafuta namna bora ya ukuaji uchumi kupitia sekta ya uvuvi.

“Sisi tuko katika hatua nzuri ya kuweza kukamilisha ujenzi wa bandari ya uvuvi, tukishafanikiwa kujenga bandari ya uvuvi, maana yake ni kwamba meli zitatia nanga hapa kwetu, tutapata ajira, tutatengeneza pia vile vile  maeneo ya kuhifadhia samaki kwa wingi, tutachakata, tutakuwa na uwezo wa kuuza katika soko la ndani na soko la nje.” Alisema Mhe. Ulega

Aidha, amesema serikali imeshaanza hatua ya ununuzi wa meli zake zenyewe, hatua iliyoilazimu kulifufua Shirika la Uvuvi (TAFICO) ambalo tayari limeshaanza kufanya kazi.

“Ili uchumi wenyewe uwe endelevu ni lazima kulinda mazingira ya bahari, maziwa, mito, kulinda rasilimali zilizopo humo, ndio maana Tanzania inafanya kazi ya ulinzi wa rasilimali hizo ili ziwe endelevu hata kwa vizazi vijavyo viweze kukuta na kuzuia uchafuzi wa mazingira hayo pamoja na uvuvi usiofuata sheria.” Alisema Mhe. Ulega

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema pia katika mkutano huo wa ‘Blue Economy’ wenye lengo la kukuza uchumi kupitia sekta ya uvuvi uliofanyika Mjini Nairobi nchini Kenya, umebainisha kuwa sekta ya utalii ni muhimu katika uchumi endelevu, sambamba na ulinzi na usalama wa nchi, pia kuzuia uingizwaji wa dawa za kulevya ambazo zimekuwa zikiingizwa katika mataifa mbalimbali kupitia njia ya bahari.

Mwisho.
Imetolewa na: Edward Kondela
Afisa Habari-Wizara ya Mifugo na Uvuvi
28.11.2018


from MPEKUZI

Comments