Rufaa Ya Mbowe na Ester Matiko Yaanza Kusikilizwa

Rufaa ya dhamana ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko imeanza kusikilizwa leo asubuhi Alhamisi Novemba 29, 2018 baada ya Jaji Sam Rumanyika kuingia mahakamani.

Hata hivyo,  upande wa mashtaka umewasilisha pingamizi la awali wakiomba rufaa hiyo itupiliwe mbali wakitoa hoja tatu za kisheria.

Kufuatia hilo mahakama imeamua kuanza kusikiliza pingamizi hilo kabla ya kuendelea na rufaa.

Mbowe na Matiko walipoingia  katika ukumbi wa Mahakama Kuu wafuasi na wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania walisimama kama ishara ya kuwapa heshima.

Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai na Matiko wamekata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.

Tayari mawakili wa pande zote wameshaingia katika ukumbi wa mahakama ya wazi namba moja.

Wabunge mbalimbali wa Chadema akiwemo Godbless Lema (Arusha Mjini) na wanachama wanaendelea kumiminika mahakamani kufuatilia mwenendo wa rufaa hiyo.


from MPEKUZI

Comments