Serikali ya Tanzania imesema itagharamia matibabu ya majeruhi watatu wa ajali iliyohusisha mabasi mawili aina ya Toyota Hiace iliyosababisha vifo vya watu 16.
Mbali na kugharamia matibabu hayo, pia mkemia mkuu wa Serikali ataongoza kazi ya uchunguzi wa vinasaba kwa ajili ya kuwatambua marehemu wa ajali hiyo.
Ajali hiyo ilitokea Jumatatu wiki hii katika kijiji cha Komaswa wilayani Tarime baada ya mabasi hayo yanayofanya safari zake kati ya Musoma-Tarime, Tarime- Rorya kugongana uso kwa uso na kuwaka moto.
Akizungumza jana katika mazishi ya pamoja ya miili 14 ambayo haikutambulika kati ya 16 ya ajali hiyo katika kijiji cha Komaswa, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema majeruhi watatibiwa hospitali yoyote nchini kulingana na maelezo ya madaktari.
Kuhusu uchunguzi wa vinasaba, Ummy alisema wizara yake imeamua kumleta mkemia mkuu kuhakikisha utambuzi wa miili ya marehemu unafanyika kwa haraka na kwa uhakika zaidi.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema asilimia 80 ya ajali zinazotokea nchini husababishwa na uzembe hasa wa madereva na amewataka kuwa makini wanapotekeleza majukumu yao. Akizungumzia ajali hiyo alisema ingawa uchunguzi bado unafanyika, taarifa za awali zinaonyesha kuwa siku ya tukio kulikuwa na mvua kubwa pamoja na ukungu hivyo upo uwezekano wa madereva hao kuwa walishindwa kuona mbele na magari hayo kugongana uso kwa uso.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema Serikali imetoa ubani wa Sh300,000 kwa kila familia iliyopoteza ndugu katika ajali hiyo.
Mkazi wa Kijiji cha Komaswa, Nyange Chacha aliyesaidia kuwaokoa majeruhi wa ajali hiyo alisema alitumia panga kukata kamba zilizokuwa zimefungwa katika moja ya magari hayo, kufanikiwa kuwatoa abiria wanne.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment