Mahakama Yapokea Hati 8 za Viwanja vya Aliyekuwa Mhasibu TAKUKURU

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana Jumanne Novemba 27, 2018 ilipokea hati nane za viwanja vinavyodaiwa kumilikiwa na aliyekuwa  mhasibu mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai.

Gugai anakabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato chake katika Mahakama hiyo.

Hati hizo ambazo ni moja ya mali anazotuhumiwa kumiliki Gugai katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani,  zilitolewa mahakamani hapo kama kielelezo baada ya shahidi wa nne wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wake dhidi ya Gugai.

Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Awamu Mbagwa akisaidiana na Vitalis Peter, alidai mbele ya hakimu Mkazi Mkuu,  Thomas Simba  kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi na upande wa mashtaka wana shahidi kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Shahidi huyo, Joanitha Kazinja kutoka ofisi ya msajili wa Ardhi,  aliwasilisha mahakamani hapo majalada nane ya hati za viwanja vya Gugai, ambavyo anadaiwa kumiliki.

Kazinja ambaye ni msajili wa hati msaidizi  kutoka wizara hiyo, alidai Gugai ni mmoja wa wamiliki walioandikishwa katika kumbukumbu za hati za ardhi ambao wamesajiliwa na wizara ya Ardhi.

"Naomba majalada haya ya hati za viwanja yapokelewe na mahakama kama kielelezo ili yaweze kutumika katika ushahidi huu" Alidai Kazinja.

Baada ya mahakama kuyapokea majalada hayo,  Kazinja alianza kuchambua jalada moja baada ya jingine kwa kuieleza mahakama kuwa hati hizo zimeanza kumilikiwa lini na zipo maeneo gani.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Washtakiwa hao wanatetewa na jopo la mawakili  Alex Mgongolwa, Semi Malimi, Denis Tumaini, Nduluma Majembe na John Mhozya.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali ambalo linamkabili Gugai.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, akidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

 Inadaiwa kuwa akiwa Takukuru Dar es Salaam, Gugai alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni ambazo hazilingani na kipato chake huku akishindwa kuzitolea maelezo.


from MPEKUZI

Comments