Lukuvi atangaza kiama wenye viwanja visivyoendelezwa Dar

 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametangaza kiama kwa walionunua viwanja katika mradi wa viwanja 20,000  jijini Dar es Salaam, akisema visivyo na uzio mwisho wa kuvimiliki ni Desemba 2018.

Amesema ukifika muda huo vitakavyobainika kutoendelezwa Serikali itavichukua bila fidia yoyote.

Viwanja hivyo ni vile vilivyopo maeneo ya Bunju, Mpiji, Toangoma,  Mwanagati, Kibada, Gezaulole Mwongozo, Mbweni na Mbweni Malindi jijini Dar es Salaam.

Lukuvi ametoa kauli hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 29, 2018 jijini Dar es Salaam.

Amesema mradi wa viwanja hivyo ulisimamiwa na Serikali na viliuzwa kwa wahusika na kwamba zaidi ya asilimia 50 havijajengwa wala kuendelezwa.

"Wale wachache waliojenga hawakai kwa raha kuna watu wanawavamia na kuwasumbua, hivyo watakwenda kuvifuatilia na kujua wamiliki ni kina nani,” amesema.

"Nitamsamehe yule tu aliyeweka angalau uzio, tofauti na hapo Desemba mwisho wao navichukua.”


from MPEKUZI

Comments