Lukuvi Aipiga Kufuri Idara ya Ardhi Dar....Aagiza Watumishi Wote Warudishwe Wizarani Kupangiwa Majukumu Mengine
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, amefanya uamuzi mgumu kwa kuifuta Idara ya Ardhi iliyokuwa katika ofisi za Jiji la Dar es Salaam na kuamuru watumishi wote waliokuwa katika idara hiyo, kurudishwa wizarani kupangiwa kazi nyingine.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara katika ofisi za Jiji jana, Lukuvi alisema Idara ya Ardhi ya Jiji imekuwa chimbuko la utapeli wa ardhi katika jiji hilo.
“Hapa ndio chimbuko la utapeli wa ardhi, wizi, kuonea maskini hasa viwanja vya Mbezi na Tegeta, kwa kupitia ofa, ilimradi mtu ajifunze kuandika mwaka wa nyuma sana,” alisema Waziri Lukuvi.
Alisema mawasiliano ya ardhi ya Dar es Salaam yatafanywa na manispaa husika kupitia mkoani hadi wizarani na siyo jiji tena.
“Hawa wa Jiji wataendelea kushughulika na shughuli zao nyingine tu walizopangiwa kwa sababu hawamilikishi, hawana ardhi, hawapangi, hawapimi, kwa hiyo watumishi wote waliopo hapa wa sekta ya ardhi, kesho (leo) wakaripoti kwa Kamishna wa Kanda, watapangiwa kazi nyingine na hata ofisi ya masijala ya hapa naifunga leo (jana),” alisema Lukuvi.
Alisema ili kupunguza migogoro ya ardhi, wizara inatarajia kuweka nyaraka zote za ardhi katika Jiji la Dar es Salaam katika mfumo wa kielektroniki kuanzia mwezi ujao.
“Tangu nimeanza kazi hii mwaka 2015 katika Wizara hii ya Ardhi, nimekuwa napambana sana na matapeli na udanganyifu wa ardhi katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini leo nimefikia kwenye chimbuko la udanganyifu mkubwa linatoka kwenye ofisi ya Jiji, nyaraka za jiji ndizo zinasababisha udanganyifu,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Jiji la Dar es Salaam halina ardhi, halipangi, halipimi, halimilikishi, halikusanyi kodi, lakini bado wanaendelea kutoa ofa za umiliki wa ardhi na ndizo zinatusumbua sana, na inawezekana hazitolewi na Jiji, lakini huko mtaani zinatolewa sana, wakati hawana mamlaka ya kufanya hivyo,” alisema.
Alisema ofa hizo hazina uhalali wa kumilikisha ardhi, lakini bado zimeendelea kutolewa, hivyo kuongeza migogoro katika ardhi.
Alisema kuanzia sasa mtu yeyote ambaye anamiliki ardhi kupitia ofa hiyo haitatambulika tena na kuwaomba maofisa ardhi katika Mkoa wa Dar es Salaam kutozitambua zinazokuwa na mhuri wa Jiji hilo.
“Kuna watu wamekaa mkao wa kula hapa Dar es Salaam, kazi ni kuchapisha ofa za Jiji kwa viwanja ambavyo vimeshamilikishwa na mamlaka za Manispaa, ilimradi tu kutuchanganya.
"Na nilishatoa muda katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kwamba kila mtu anayemiliki ardhi kwa ofa kufanya mpango wa kupata hati, wale ambao bado wamebaki na makaratasi haya ya hati imekula kwao, hakuna ofisa ardhi atakayepokea ofa kwa sasa, na mtu asinunue kiwanja chenye ofa haipo,” alisema Lukuvi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji hilo, Sipora Liana, alisema wameshaanza kuhamisha nyaraka za ardhi kupeleka katika wilaya hizo.
“Kwa sasa tunapeleka mafaili yenye nyaraka za ardhi kila sehemu yanakohusika kama ni Temeke, Kinondoni, Ilala na Kigamboni,” alisema Liana.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment