Kubenea Apangua Kauli ya Makonda

Mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Saed Kubenea amefunguka juu ya tuhuma za Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kumchonganisha na wananchi wake kwa Rais Magufuli.

Kubenea amesema kuwa kabla ya kutoa kauli ile mbele ya Rais alipaswa kumtafuta ili kujua ni kwanini hajafika katika hafla ile ya uzinduzi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).

Kubenea amesema kuwa amesikitishwa na kitendo cha kiongozi huyo kuzungumza bila kuwa na taarifa sahihi kuhusiana na sababu za kutofika kwenye uzinduzi huo.

"Imekuwa kawaida yake kuchonganisha watu bila kuwa na sababu za msingi, kama alifahamu ujio wa Rais pale alishindwa nini kunitafuta kabla?, Unajua unaweza sema neno juu ya mtu kumbe ana matatizo yaliyosababisha asifike", amesema Kubenea.

Kubenea amesema kuwa kilichomkwamisha kufika katika uzinduzi huo alikuwa katika kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Ubungo na hakufahamu kama itakuwa ni hafla ya muda mfupi na jiografia ya halmashauri iko mbali.

Jana katika hafla ya uzinduzi wa maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Makonda alisema kuwa ameshangazwa na kutokuwepo kwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea mahala ambapo Chuo kinapatikana katika Jimbo lake, pamoja na majirani zake ambao ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

"Nashangaa hata wale wabunge wapinzani wa Dar es salaam ambao mara nyingi wanakuja vyuoni kuwarubuni wanafunzi wawapigie kura lakini hawatokei kwenye shughuli za maendeleo, kazi yao ni kukosoa tu", amesema Makonda.


from MPEKUZI

Comments