Jebra Kambole, wakili wa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe anayeshikiliwa na polisi kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam, amesema mwanasiasa huyo amenyimwa dhamana.
“Polisi wamesema hawawezi kumuachia kwa leo wanaendelea kumshikilia kwa ajili ya mahojiano. Wamesema hawawezi kumpa dhamana,” amesema Kambole .
Zitto alikamatwa na polisi leo saa 5 asubuhi na kupelekwa kituo cha polisi Oysterbay ambako alihojiwa kwa takribani saa tatu, kisha kuhamishiwa kituo kikuu cha polisi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Liberatus Sabas leo amewaeleza wanahabari kuwa wanamshikilia Zitto kutokana na matamshi aliyoyatoa hivi karibuni.
Jana, Jeshi la Polisi mkoani Kigoma lilimtaka Zitto kuwasilisha vielelezo juu ya kauli aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari Jumapili iliyopita Oktoba 28, 2018 kuwa ana taarifa za wananchi zaidi ya 100 kuuawa katika tukio la mapigano ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi wilaya ya Uvinza mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno amesema tuhuma za mbunge huyo hazina ukweli wowote na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.
Katika ufafanuzi wake leo, Kambole amesema Zitto alipofikishwa Oysterbay aliandika maelezo, kuhojiwa akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi.
“Baada ya kuhojiwa aliandika maelezo ya awali na aliwaeleza kuwa kama kuna maelezo mengine atayatoa mahakamani,” amesema Kambole.
“Hakuna chochote kilichoendelea na sheria inamruhusu kama unaona hulazimiki kutoa maelezo. Maelezo kuhusu makosa yake hajayatoa na hakulazimishwa kuyatoa anasubiri kama akipelekwa mahakamani atayatoa huko.”
Ameongeza, “Wamesema dhamana yake wameishikilia na kosa lake ni kutoa maneno ya kichochezi.”
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment