Waziri wa Kilimo: Hatuwezi Kuendelea Kuagiza Sukari Wakati Tuna Uwezo Wa Kufanikisha Uzalishaji

Na Mathias Canal-WK, Dodoma
Serikali imeipa changamoto Bodi ya sukari nchini kutekeleza majukumu yake kwa weledi ikiwa ni pamoja na kusisitiza kuhuisha uzalishaji wa sukari kwa wingi ili kuondokana na uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.

Kampuni mbalimbali za uzalishaji wa sukari nchini zimeitikia wito wa Serikali wa kuongeza uzalishaji wa sukari ili nchi iweze kujitegemea kwa bidhaa hiyo pendwa kwa matumizi ya nyumbani na viwandani na ziada jambo litalopelekea Bodi ya sukari kusimamia majukumu yake ipasavyo ili kuondokana na uagizaji wa sukari nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo jumatatu tarehe 29 Octoba 2018 na Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb)  wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Mjini Dodoma.

Waziri Tizeba amemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari nchini Bi Mwamini Juma Malemi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Kenneth Michael Kitundu Bengesi Kudhibiti sukari inayoingia nchini pasina utaratibu huku akiwataka kusimamia kwa weledi ufanisi katika uongezaji wa uzalishaji wa sukari nchini.

Aidha, Dkt Tizeba alisema kuwa ufungashaji wa sukari kwenye ujazo wowote ule kwa kutumia vifungashio vya aina yoyote kama vile mifuko yenye nembo ya SUPER FINE lazima uzingatie Sheria ya Sukari Namba 26 ya Mwaka 2001 ambayo inazuia ufungashaji wa sukari bila kupata idhini ya Bodi ya Sukari Tanzania.

Alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria hiyo ni marufuku kufungasha au kuuza sukari nyeupe kwa kuwa sukari hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya viwandani kama malighafi na sio kwa ajili ya matumizi ya kawaida majumbani.

Alisisitiza kuwa Mtu yeyote atakayebainika kuvunja Sheria hiyo ya Sukari, atawajibika kulipa faini ya kiasi cha fedha kisichopungua Shilingi Milioni Kumi (10,000,000) au kifungo cha miaka mitatu (3) jela au vyote kwa pamoja.

“Kuna watu wanaolipa kodi ili wazalishe sukari lakini inapoingia sukari ambayo imepenya kinyemela hata ulinganifu wa soko madukani unakuwa mdogo kwa kuwa wanaoingiza bila utaratibu wanauza kwa kiasi cha chini kwa kuwa hawana uchungu wa kulipa kodi”

“Na hili sio jambo la hiara Bodi ni lazima isimame kidete kubaini mianya yote ya wafanyabiashara wanaoingiza sukari bila utaratibu” Alikaririwa Dkt Tizeba

Kuhusu sukari ya viwandani (Industial Sugar) Dkt Tizeba alisema kuwa, wafanyabiashara wamekuwa wakiomba kiwango kikubwa cha kibali cha uagizaji wa sukari lakini serikali ikihakiki kupitia kodi waliyolipa inakuwa haifanani na kiasi kilichoagizwa.


from MPEKUZI

Comments