Rais Magufuli Amlilia Isack Gamba, Mwili wake Kusafirishwa Leo Kuelekea Jijini Mwanza

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ametoa salamu za pole kwa walioguswa na msiba wa aliyekuwa mtangazaji wa kituo cha idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani DW, Isack Gamba.

Akitoa salamu za Rais Magufuli wakati wa zoezi la kuaga mwili Isack katika viwanja vya Lugalo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa mawasiliano ikulu Gerson Msigwa amesema Rais Magufuli ameguswa na msiba huo.

Msigwa amesema; “kwa niaba ya Rais napenda kutoa pole kwa familia ya Isack Gamba, na wote ambao mmekusanyika hapa, niseme tu mheshimiwa Rais anawapa pole sana na amesema anatupenda na anafuatilia kazi zetu na kazi kubwa tunazofanya kwenye kutimiza malengo ya nchi.”

“Alitamani sana kuwepo kwenye msiba wa Isack Gamba lakini bahati mbaya majukumu yamembana ameshindwa kuja na anamwombea heri Mungu amlaze mahali pema peponi”, ameongeza Msigwa.

Awali mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ameiomba idhaa ya Kiswahili ya DW kuwaangalia wanahabari wa kitanzania ili kuziba pengo la Isack Gamba.

“Niwaombe ndugu zangu wa ujerumani nafasi aliyokuwa Isack irudi kwenye nchi ili tusipoteze nafasi hiyo niwaombe mtakapofika kwenye ujazaji wa nafasi hiyo muangalie vijana wa kitanzania”, amesema Paul Makonda.

Mwili wa Isack Gamba unatarajiwa kusafirishwa leo kuelekea mkoani Mwanza na baadaye kuelekea Bunda kwaajili ya mazishi.


from MPEKUZI

Comments