JWTZ Kuwa Mwenyeji Wa Mazoezi Ya Majeshi Ya Nchi Za Jumuiya Ya Afrika Mashariki Mkoani Tanga

Jeshi  la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanatarajia kuwa wenyeji wa zoezi la mafunzo yaitwayo Ushirikiano imara 2018 litakaloshirikisha nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda ambapo mafunzo yataendeshwa mkoani Tanga .

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam Mkuu wa Mafunzo na Operesheni  (JWTZ) Meja Jenerali Alfred Fabian Kapinga amesema kuwa, zoezi hilo ni la medani na litafanyika katika wilaya za mijini pamoja na Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Ameeleza kuwa zoezi hilo litaanza rasmi tarehe 05 mpaka 21, sambamba na hilo mafunzo hayo yatalenga kujenga uwezo wa kukabiliana na uharifu pamoja na majanga.

Pia amesema kuwa dhumuni la zoezi hilo kikanda ni kubadilishana uzoefu wa kiutendaji, kuimarisha mahusiano baina ya nchi, majeshi ya Afrika Mashariki pamoja na taasisi zingine za kiraia ambazo zitashiriki zoezi hilo.

Sanjari na hilo kutakuwa na kazi za kusaidia jamii katika shughuli mbalimbali zikiwemo ujenzi wa madarasa, ofisi za walimu pamoja na vyoo katika Shule ya msingi ya Machemba iliyopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, pia kutakuwa na utoaji wa huduma za tiba kwa wananchi katika eneo la zoezi.

Hivyo, Meja Fabian ametoa rai kwa wakazi wa Tanga kuonyesha ukarimu pamoja na amani baina ya wageni watakaokua kwa kipindi chote cha mafunzo kama walivoonyesha mwaka jana ambapo mafunzo yalikua yakiendeshwa.


from MPEKUZI

Comments