Waziri Kalemani Azindua Matumizi ya Gesi Asilia Katika Kiwanda Cha Dangote

Waziri  wa Nishati, Dk Medard Kalemani jana amezindua mradi wa kuunganisha miundombinu ya gesi asilia kwa kiwanda cha saruji cha Dangote, hivyo sasa kuwezesha uzalishaji mkubwa kufanyika ambao utapunguza gharama za uzalishaji na hivyo kushusha bei ya saruji.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dk Kalemani alisema Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuhakikisha kila mwananchi anakua kiuchumi kutoka uchumi mdogo na kufikia mkubwa hasa nchi inavyoelekea kwenye uchumi wa viwanda, hivyo kuongezeka kwa uzalishaji wa saruji hapo ni fursa kubwa kwa wana-Mtwara na maeneo mengine nchini.

Mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili, ya kwanza ikiwa ni kuunganishwa kwa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji wa umeme unaofikia megawati 45 utakaozalishwa kwenye mashine tatu zenye uwezo wa kuzalisha megawati 15 kwa moja. Hivyo, alisema kutokana na uwapo wa gesi hiyo kutasababisha uzalishaji huo kuwa mkubwa na utaleta mabadiliko ya kimaendeleo mkoani hapa.

“Kubwa niwaombe wananchi kutunza miundombinu yetu ili iweze kudumu na iweze kutusaidia kukuza zaidi uchumi wetu” alisema Dk Kalemani. 

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert alisema mradi huo unatarajia kusafirisha kiasi cha futi za ujazo milioni 30 za gesi asilia kwa siku, ambacho kitatumika kuendeshea mitambo ya kuzalishia saruji hadi ifikapo Novemba mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho cha Dangote, Jagat Rathee alisema kuwepo kwa gesi hiyo kiwandani hapo kwa hivi sasa kutachochea mafanikio mkubwa kutokana kutapunguza gharama ya uzalishaji wa saruji ikilinganishwa na hapo awali, lakini pia kuongezeka kwa uzalishaji kwa jumla.


from MPEKUZI

Comments