Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wataalamu wa kitanzania kutokuwa chanzo cha kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini yenye lengo la kuleta maendeleo kwa taifa.
Akizungumza leo Alhamisi (Septemba 27, 2018) Jijini Dar es salaam, wakati akifungua rasmi barabara ya juu ya Patrick Mfugale iliyopo katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, Rais Magufuli alitoa wito kwa wataalamu wa kitanzania wasiwe chanzo cha kukwamisha miradi mbalimbali kwa kuwa miradi hiyo ina lengo la kuwasaidia Watanzania.
“Wataalamu wasiwe chanzo cha kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa, ni lazima tuweke maslahi yetu kwanza, tusitumike kukwamisha kutekeleza miradi itakayoasaidia Watanzania” alisisitiza Rais Magufuli
Aidha, Rais Magufuli alimpongeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale na kusema kuwa anamfahamu mhandisi huyo kama mtu mzalendo, mwaminifu, mwadilifu na mchapakazi.
“Nampongeza Mtendaji Mkuu Mfugale kwa kubuni, kuandaa mchoro wa barabara hii, ambapo pia amebuni michoro ya daraja la Mkapa lenye urefu wa km 10, ambalo ni daraja refu kuliko yote katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati” alisema Rais Magufuli.
Vilevile, Rais Magufuli aliishukuru Serikali ya Japan kwa kutoa msaada ulioasaidia katika ujenzi wa barabara hiyo, na kusema kuwa ni misaada inayolenga kutatua changamoto yenye kuleta mabadiliko ya kweli.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale alisema kuwa barabara hiyo inayojulikana kama barabara ya juu ya Mfugale yenye urefu wa takribani kilomita moja, imefanikiwa kupunguza msongamano wa magari kwa asilimia 100 kutoka Airport kuelekea mjini na asilimia 50 kutoka Bandarini kuelekea Ubungo.
Naye, Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA),Toshio Nagase aliipongeza kampuni za Japan na Tanzania ambazo zimeshirikiana katika ujenzi wa barabara hiyo kwa kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia kwa wakati na kutopata ajali yoyote wakati wa utekelezaji wake.
“Najivunia uwepo wenu katika mradi huu, hii imeonesha ushirikiano na urafiki mkubwa uliopo kati ya nchi za Tanzania na Japan, pia mmefanikiwa kukamilisha mradi huu kwa kutumia masaa 2, 100,000 ya ujenzi bila kupata ajali yoyote na umekabidhiwa kwa Watanzania kama ilivyopangwa” alisema Nagase
Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Balozi Masaharu Yoshida alisema kuwa barabara hiyo imepunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa, itasaidia ukuaji wa uchumi kwa vile inarahisisha usafirishaji wa watu na mizigo.
Aidha, aliongeza kuwa mradi huo ni alama muhimu ya urafiki na uhusiano wa kudumu kati ya nchi za Tanzania na Japan.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya juu ya Mfugale ulianza kujengwa mwaka 2016, kwa kutumia fedha za mkopo wa nchi ya Japan na kiasi kingine kikiwa ni fedha kilitolewa na Serikali ya Tanzania.
Barabara hiyo yenye mita 425, imejengwa kwa kutumia nguzo kubwa sita, ina urefu wa kilomita moja, yenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 180 kwa wakati mmoja.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment