Mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji (ICSID) imeikataa rufaa ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupinga hukumu ya kuilipa Benki ya Standard Chartered Dola 148.4 milioni za Marekani (Sh336 bilioni).
Hata hivyo, si Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka wala msemaji wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Maura Mwingira walioeleza kufahamu kuhusu hukumu hiyo.
Akiongoza jopo la wajumbe waliosikiliza rufaa hiyo, Rais wa ICSID, Claus von Wobeser ametupilia mbali hoja za Tanesco za kuitaka mahakama hiyo kutengua uamuzi wa awali ulioipa ushindi benki hiyo ya Hong Kong.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Tanesco kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa mwaka 2016 ikilitaka shirika hilo kulipa kiasi hicho cha fedha.
Fedha hizo ni madai ya malipo ya umeme baina ya Tanesco na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) iliyopewa zabuni ya kufua umeme wa dharura kuanzia Mei 26, 1995 huku ikidaiwa na benki hiyo.
IPTL ilikuwa ikidaiwa na benki hiyo ya Hong Kong kutokana na mkopo iliyochukua kutekeleza mkataba kati yake na Tanesco.
Mahakama hiyo imetupilia mbali madai yote ya Tanesco kupinga hukumu hiyo na kuitaka ilipe fedha kama ilivyoamriwa katika hukumu ilitolewa mwaka 2016.
Tanesco katika nakala ya hukumu hiyo ya Agosti 2 imeagizwa kulipa gharama zote za uendeshaji wa shauri hilo ikiwamo ada ya kesi na malipo ya wajumbe wa kamati waliolisikiliza.
Tanesco katika shauri hilo iliwakilishwa na mawakili Richard Rweyongeza wa kampuni ya R.K. Rweyongeza & Co Advocate; Beredy Maregesi (Crax Law Partners); David Hesse, Devika Khanna, Thomas Roberts na Nefeli Lamrou wa kampuni ya Clyde & Co ya Uingereza. Usikilizaji wa shauri hilo ulifanyika Novemba 27 na 28 mwaka jana.
Crtedit: Mwananchi
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment