TAMWA Yalaani Vipigo Kwa Wanafunzi

Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (Tamwa), kimelaani vitendo na matukio ya ukatili unaofanywa na baadhi ya walimu kuwapiga wanafunzi bila kufuata sheria na kusababisha baadhi yao kuathirika kisaikolojia na hata kupoteza maisha.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga, imesema miongoni mwa matukio ya kusikitisha ni lile la Agosti 27 mwaka hu ambapo mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibeta, Bukoba mkoani Kagera, Sperius Eradius (13) alifariki dunia baada ya kupigwa na mwalimu wake kwa kutuhumiwa kuiba pochi ya mwalimu.

Amesema Sheria juu ya viboko mashuleni katika Kifungu cha 61(1)(v) cha Sheria ya Elimu Sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002, kinampa mamlaka waziri wa huyo kufanya hivo.

“Tukio jingine ni lile la mwaka 2016 lililotokea kwa msichana wa kidato cha nne (17) aliyekuwa akisoma katika shule moja ya sekondari ya kata mkoani Mbeya ambaye alivuliwa nguo zake za ndani na kucharazwa bakora zisizo na idadi kwa sababu za utoro shuleni, adhabu iliyotolewa na walimu wanne wa shule hiyo akiwemo mkuu wa shule hiyo.

“Sheria inamtaka mwalimu mkuu wa shule husika kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo, Mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakuwa na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika.

“Tamwa inalaani kwa nguvu ukatili wa aina hii na ni matarajio yetu kuwa vipigo na mauaji mashuleni havitatokea tena,” amesema.


from MPEKUZI

Comments