Sugu Alivyomwaga Machozi Akisoma Wasifu wa Mama Yake....."Afya ya Mama Ilibadilika Baada ya Mimi Kufungwa"

Wasifu wa Desderia  Mbilinyi (61) ambaye ni mama mzazi wa  Joseph Mbilinyi 'Sugu' umewatoa machozi waombolezaji.

Sugu ambaye ni mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), alishindwa kujizuia kutokwa na machozi wakati akisoma wasifu wa mama yake.

Hilo lilijiri  jana Agosti 28, katika Kanisa Katoliki lililopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.

Akisoma wasifu wa Desderia aliyezaliwa Desemba 25, 1956, Sugu alisema maisha ya mama yake kwa sehemu kubwa alikuwa mkulima mdogo na alikuwa mjane toka mwaka 1992.

“Mama alikataa kuolewa tena na kujikita kanisani akiwa ni mwana Karistimatiki Katoliki.

“Februari (2018) wiki moja baada ya mimi (Sugu) kufungwa, mama yangu bado aliendelea kuamini kuwa nilifungwa kwa kuonewa,” alisema Sugu.

Alisema baada ya hapo, afya ya mama yake ilibadilika na alianza kuugua shinikizo la damu lililozidisha tatizo alilokuwa nalo awali la figo.

Alisema mama yake alianza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Julai alihamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi hadi Agosti 26, alipofariki dunia.

Sugu akitumia Biblia, alisoma Waraka wa Timotheo 4:7 na kusema “Mama yangu amevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo ameumaliza, Imani ameilinda."

Baada ya kusema hivyo alishindwa kuendelea kuusoma wasifu huo na kububujikwa machozi, hali iliyosababisha waombolezaji wengine nao kuanza kutokwa na machozi.

Desderia ameacha watoto wa kuzaa watano na wa mumewe watatu.

"Natoa shukrani kwa madaktari wa Rufaa Mbeya, Taasisi ya Jakaya Kikwete na Kitengo cha Figo hapa Muhimbili," alisema Sugu.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria misa hiyo ya maziko ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar,  Salum Mwalimu.

Desderia anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake jijini Mbeya leo .


from MPEKUZI

Comments