PICHA: Rais Uhuru Kenyatta Alivyokutana na Trump Ikulu ya Marekani

Rais Donald Trump wa Marekani amekutana na mwezake wa Kenya Uhuru Kenyatta mjini Washington na kuzungumzia masuala mbalimbali, zaidi wakiangazia biashara na usalama.

Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu ya Marekani, wakati wa ziara hiyo mataifa hayo mawili yalikubaliana na kutangaza mikataba ya jumla ya $900 milioni.

Rais Kenyatta ni kiongozi wa tatu kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara kukaribishwa Ikulu ya White House na kufanya mazungumzo na Rais Trump.

"Tumekuwa na ushirikiano mzuri na wa kipekee na Marekani katika masuala ya usalama na ulinzi, hasa katika harakati za kukabiliana na ugaidi. Muhimu zaidi tuko hapa kuboresha ufungamano wetu katika biashara na uekezaji, " kasema Rais Kenyatta.

Rais Trump alisema Kenya na Marekani zitaendelea kushirikiana kuimarisha ufungamano wao katika biashara, uekezaji na usalama.

"Tunafanya shughuli nyingi za utalii, biashara na ulinzi. Na kwa wakati huu tunajibidiisha kuboresha usalama," alisema Rais Trump. " Tunafurahia sana kuwa nawe hapa."

Miongoni mwa mengine, Bw Trump alifurahia pendekezo lililowasilishwa na kampuni ya ujenzi kutoka Marekani Bechtel Corporation kutaka kupewa kandarasi ya ujenzi wa barabara ya kisasa ya kutoka Nairobi kwenda Mombasa.

Mataifa yote mawili yalikubaliana na kuendelea na mashauriano zaidi ili kuafikiana kuhusu ufadhili wa ujenzi huo.

Viongozi hao wawili walijadiliana pia kuhusu safari za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi New York zitakazoanza mwezi Oktoba mwaka huu na kukubaliana kwamba safari hizo za ndege zitaimarisha zaidi utalii na biashara kwa manufaa ya nchi hizi mbili.

Marekani ndiyo chanzo kikuu cha watalii wanaozuru Kenya na taifa hilo la Afrika Mashariki linatarajia kutumia fursa ya safari za moja kwa moja za ndege za Kenya Airways kati ya mataifa hayo mawili ambazo zitaanza Oktoba 28 kuimarisha idadi ya watalii wanaofika kenya.

Viongozi hao wawili kwa pamoja wamejadili njia za pamoja za kupambana na ugaidi na ushirikiano wa kibiashara. Mpango wa upanuzi wa barabara inayohusisha miji mikubwa ya Kenya, Mombasa na Nairobi pia ilijadiliwa.



from MPEKUZI

Comments