Mzee Mwinyi Amuombea Dua Na Kumjulia Hali Dkt.kigwangalla MOI

RAIS Mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi leo Agosti 29,2018 amemtembea na kumuombea dua maalum Dkt Hamisi Kigwangalla ambaye anapata matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI akiuguza majeraha ya mkono aliyopata katika ajali iliyotokea Agosti 4, mwaka huu Mkoani Manyara.

Mzee Mwinyi aliambatana na Mkewe Bi. Siti Mwinyi ambapo wamemjulia hali pamoja na kufanya dua hiyo ili aweze kupona haraka kurejea kwenye majukumu yake ya kitaifa.

“Nimefika leo kukujulia hali na upokee dua hii upone haraka. Sisi tunaendelea kukuombea muda wote kwa muumba” alieleza Mzee Mwinyi.

Kwa upande wake Dkt. Hamis Kigwangalla amemshukuru Mzee Mwinyi na Mama Mwinyi kufika kumjulia hali ambapo awali alimuelezea kuwa anaendelea vizuri na muda wowote ataruhusiwa.

“Nashukuru kufika kwenu na sasa naendelea na mzoezi vizuri huku kubwa nikisubiria ruhusa ya Madaktari wanaoendelea kunipatia matibabu” alieleza Dkt. Kigwangalla.

Katika hatua nyingine kwa sasa Dkt. Kigwangalla afya yake imeendelea kuimarika zaidi ambapo jana jioni ya Agosti 28, ameweza kutembea umbali wa zaidi ya Kilometa Nane ambapo hii ni hatua nzuri kwani kila siku amekuwa akiongeza umbali wa kutembea kwa lengo la kufanya mazoezi ya viungo vyake.

Dkt Kigwangalla alihamishiwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI tarehe 12/08/2018 baada ya kupata matibabu ya awali katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kwa sasa bado anaendelea na tiba kuuguza mkono wake wa kushoto.


from MPEKUZI

Comments