ELINIKUNDA Mushi (50) ,amefariki dunia baada ya gari la kubebea wagonjwa (ambulance) mali ya jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) , lililokuwa likimuwahisha hospital ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu kupata ajali eneo la Kibiki, kata ya Bwilingu, Chalinze mkoani Pwani.
Katika ajali hiyo watu wengine wanne walijeruhiwa baada ya dereva wa ambulance kudaiwa kuligonga gari nyingine kwa nyuma,lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara kwa ajili ya matengenezo .
Akitoa taarifa kuhusu tukio hilo, kamanda wa polisi mkoani Pwani, (ACP) Wankyo Nyigesa ,alisema ajali hiyo imetokea alfajiri agost 31 mwaka huu.
Alieleza, gari namba 3489 JW 12 aina ya Ashok Leyland inayomilikiwa na kikosi cha jeshi 911 KJ cha Ihumwa Dodoma, mali ya JWTZ, lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Dar es salaam aliligonga gari lingine lenye namba za usajili T. 764 ACK aina ya Toyota canter na kusababisha kifo cha mtu mmoja .
Nyigesa alisema, aliyepoteza maisha ni Elinikunda ambae alikuwa mgonjwa akipelekwa kwenye matibabu katika hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Watu wanne walijeruhiwa ambao ni pamoja na Beatrice Shidodolo (56)muuguzi wa hospital ya Dodoma, Ufo Swai (48) mkazi wa Ngerengere yeye alikuwa akimhudumia mgonjwa akiwa Dodoma “alisema Nyigesa.
Nyigesa aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Justine Patrick (28)ambae alikuwa dereva wa gari namba T. 764 ACK iliyokuwa imeegeshwa kwa matengenezo na Rashid Rais (35) alikuwa fundi wa gari hilo wakazi wa Chalinze.
Uchunguzi wa awali umebaini katika ambulance hiyo ilikuwa imepakia watu wengine wanne ambao hawakuweza kupata majeraha yoyote ambao ni MT. 3480 SGT Elimasa Mushi (40) askari wa JWTZ makao makuu ya Jeshi (MMJ).
Nyigesa aliwataja wengine kuwa ni MT 95881 PTE Taulin Kaira (30) askari wa 911 KJ aliyekuwa msindikizaji wa gari hilo la wagonjwa, Eveline Stanley (25) alipewa msaada wa usafiri na mtoto wake wa miezi 11 anaitwa Nicholous Petro na dereva wa gari hilo MT. 67451 SGT Shaban Mpwate.
Kamanda huyo alifafanua, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospital ya Jeshi ya Lugalo na majeruhi wamepelekwa katika hospital hiyo.
Dereva wa ambulance Shaban Mpwate,anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.
Nyigesa aliwaasa madereva wa magari ya dharura kama magari ya wagonjwa kuhakikisha wanachukua tahadhari kubwa wanapokuwa wamepewa kipaombele na watumiaji wengine wa barabara ili kuweza kuepuka ajali zembe.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment