Vyama vya CCM na Chadema, leo vitapimana ubavu katika uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Monduli jijini Arusha katika mikutano miwili tofauti ya kampeni.
Kampeni za ubunge wa jimbo hilo ambalo lilikuwa CCM tangu uhuru, hadi mwaka 2015 lilipochukuliwa na Chadema zinatarajiwa kuwa za aina yake.
Julai 30, aliyekuwa mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga alijiuzulu na kujiunga na CCM na chama hicho tawala kikampitisha kuwania tena ubunge wa jimbo hilo na sasa atachuana na Yonas Laiser wa Chadema.
Katika uzinduzi wa leo, Chadema watakuwa katika mji wa Mto wa Mbu, na kampeni zao zitazinduliwa na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya kampeni za Chadema katika jimbo hilo akiwa na wabunge na viongozi wengine wa chama hicho.
Upande wa CCM, kampeni zitazinduliwa na makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula, Monduli mjini.
Katika uchaguzi huo, wagombea wengine katika jimbo hilo ni Omar Kawanga (DP), Feruzi Juma (NRA), Simon Ngilisho (Demokrasia Makini), Francis Ringo (ADA-Tadea) Elizabeth Salewa(AAFP) na Wilfred Mlay (ACT-Wazalendo).
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment