Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kipo imara na kitashinda jimbo la Monduli.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amesema hayo jana wakati akizindua kampeni za jimbo la Monduli, katika Kata ya Mto wa Mbu, akiwataka wananchi kupuuza propaganda kuwa Chadema itakufa.
Lowassa huku akielezea maendeleo aliyoleta Monduli katika kipindi chake cha ubunge cha miaka 20, alisema aliingia ubunge wa Monduli kukiwa na shida ya maji, barabara, umeme na ardhi lakini alishughulikia na leo kila Mtanzania anajua.
Amesema kumekuwapo na maneno kuwa amerejea Monduli kulinda ngome ya Chadema jambo ambalo siyo sahihi.
"Chadema bado tupo imara na tutashinda," alisema Lowassa huku akishangiliwa
Lowassa alisema kitendo cha kujiuzulu aliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga kilikuwa cha hovyo na kimemuudhi na kumkasirisha sana.
“Ni aibu kubwa, siku hiyo alipokuwa anahama nilipata taarifa nikampigia simu akasema hapana mzee.
"Kinachoniudhi siyo kuondoka kwake bali sababu alizotoa kuwa eti Monduli hakuna maendeleo aseme alishindwa kuvaa viatu vyangu," alisema.
Alisema ajitokeze Kalanga kutaja wilaya yenye maendeleo kama Monduli, kwa sababu ina barabara na shule kila kata.
"Hivi huyu ana akili kweli, Monduli hatuna hospitali tumejenga hospitali ya kisasa Monduli nzuri sana kuliko pengine." alisema.
Katika mkutano huo, Lowassa ameunga mkono, tamko la Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuzuia polisi kutekeleza maagizo ya wakuu wa wilaya na mikoa kukamata watu bila sababu za msingi.
Alisema kumekuwapo na matukio ya kukamatwa watu bila sababu za msingi, hivyo uamuzi wa Lugola unapaswa kupongezwa.
Lowassa amewataka wakazi wa Monduli, kumchagua mgombea na Chadema, Yonas Laiser kwani ndiye atawaletea maendeleo.
Naye Laiser ameomba wananchi kumchagua kwani anajua kero zao na atashirikiana na Lowassa na madiwani kuzitatua.
Hata hivyo, alisema amekuwa akifuatwa kutakiwa kujiuzulu kugombea ubunge na udiwani na atapewa cheo serikalini lakini amegoma.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment