Kauli ya Simbachawene baada ya kuchaguliwa kumlithi Ghasia

Mbunge wa Kibakwe(CCM), George Simbachawene amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti huku akiahidi kuongoza kamati hiyo kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo kwa maslahi ya Taifa.

Simbachawene amechaguliwa jana kushika nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo Hawa Ghasia kujiuzulu.

Aidha Mbunge wa Maswa Mashariki (CCM)Mashimba Ndaki naye amechukua nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliyoachwa na Jitu Son ambaye pia alijiuzulu.

Akizungumzia kuchaguliwa kwake, Simbachawene amesema jana aliteuliwa na Spika wa Bunge Job Ndugai kuwa mjumbe wa kamati hiyo baada ya kuhamishwa kutoka Kamati ya Katiba na Sheria.

“Nilipofika kamati ya Bajeti nikaambiwa Mwenyekiti na Makamu wake wamejiuzulu  basi nikapata Interest ngoja nigombee na wajumbe wamenipitisha kwa kauli moja nataka niseme tu kwamba kamati ile nafahamu ni kamati muhimu katika mhimili wa bunge na serikali,”amesema.

Amesema misingi ya uendeshaji wake ipo kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria hivyo atasimamia sheria zote zinazosimamia sheria.

“Pia tutafanya majukumu yetu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo lakini pia kwa maslahi ya Taifa,”amesema.

Mwenyekiti huyo amesema haoni kama ni mzigo mkubwa sana kwake kwa kuwa anachojua kazi yake ni kukusanya mawazo ya wajumbe ili kutoa ushauri kwa sababu kazi ya Bunge ni kutoa ushauri kwa serikali.


from MPEKUZI

Comments