Mbunge wa Upinzani nchini Uganda ambaye pia ni mwanamuziki, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ambaye anadaiwa kupigwa na kuteswa baada ya kukamatwa mapema mwezi huu, inasemekana amezuiwa kuondoka kwa ajili ya kwenda kupata matibabu nje ya nchi.
Kwa mujibu wa BBC akizungumzia kukamatwa kwa mteja wake, Mwanasheria wa Mbunge huyo,Robert Amsterdam amesema Bobi Wine alizuiliwa kuingia katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Uganda na kuchukuliwa na polisi ambao wanadaiwa kumpeleka katika hospital ya serikali.
”licha ya kwamba Jaji alitaka apewe pasi yake ya kusafiria kwa sababu anahitaji kuondoka nchini humo kwa sababu ya kwenda kupata matibabu nje, kufuatia mateso makali ambapo yeye na wabunge wengine 33 wa upinzani waliyapata, amechukuliwa kikatili na gari la wagonjwa la polisi, Mawakili hawajui wapi alipopelekwa na tumepatwa na mshtuko..” Alisema wakili wa Bobi Wine
Kabla ya Kuzuiliwa kwa Bobi Wine, mbunge mwingine tena wa upinzani Francis Zake pia alizuia Uwanja wa ndege kwa ajili ya kwenda kupata matibabu nje ya nchi.
Bob Wine anakabiliwa na makosa ya uhaini, kufuatia tukio la kushambuliwa kwa mawe gari la Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni. Aliachiliwa kwa dhamana kutoka kizuizini alikokuwa akishikiliwa siku ya Jumatatu, akiwa katika hali mbaya.
Mwanasheria wake Robert Amsterdam ameongeza kuwa kipaumbele cha Bobi Wine ni kupata matibabu na si kuitoroka nchi.
”Watoto wake watabaki nchini Uganda, ni safari ya muda mfupi, kwa ajili tu ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu. Anakabiliwa na maumivu makali.”
“Anamajeraha makubwa yaliyosababishwa na kuteswa kwake na vitu vya chuma na vifaa vingine vilivyotumika kumtesea na anahitaji msaada.”
”Tuseme kuwa hakuna kiungo chake chochote cha mwili kisichouma na ana matatizo makubwa katika figo lake.”
Siku ya Jumatano Spika wa Bunge la Uganda alitaka kukamatwa kwa maafisa usalama walioshiriki kumpiga mbunge huyo.
Hata hivyo serikali ya Uganda imekataa madai kuwa Bobi Wine alitendewa vibaya wakati alipokuwa kizuizini.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment