Waziri Majaliwa Akutana Na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ujio wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa  la Mpango wa  Chakula Duniani (WFP), Bw. David Beasley  hapa nchini ni fursa itakayowawezesha Watanzania kunufaika  kwa kiwango kikubwa katika kilimo, uhifadhi na uuzaji wa mazao ya chakula yanayolimwa hapa nchini.

Akizungumza baada ya kukutana na Bw. Beasley jijini Dar es Salaam jana mchana (Ijumaa, Julai 27, 2018), Waziri Mkuu amesema Tanzania inatarajiwa kuwa na ziada ya chakula  msimu wa mavuno utakapokamilika mwaka huu hivyo itahitaji sana kupata soko nje ya nchi ili iweze kuuza ziada hiyo.

“Taarifa za Wizara ya Kilimo zinaonesha kuwa mavuno ya mazao ya chakula kama mahindi, maharage na mbaazi yatafikia tani milioni 16 wakati mahitaji ya chakula kwa Watanzania kwa mwaka ni tani milioni 13, hivyo tutakuwa na ziada ya tani milioni tatu,” amesema.

Akitoa ufafanuzi, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia Julai 2018 ambapo msimu wa mavuno bado unaoendelea, tayari nchi ina ziada ya tani milioni moja kwani taarifa za Wizara ya Kilimo zinaonyesha kuwa tayari zimekwishavunwa tani milioni 14.

Amesema hatua ya WFP kukubali kununua chakula  cha ziada kitakachozalishwa hapa nchini imewahakikishia Watanzania  kuwa mazao yao hayatakosa soko kwani utaratibu wa uuzaji na ununuzi  wa nafaka hasa mahindi unafanywa na Wizara ya Kilimo ikishirikiana na WFP.

Ili kuhakikisha usalama wa chakula kinachozalishwa nchini, Serikali inajenga maghala ya kuhifadhi nafaka kwenye mikoa minane yenye uwezo wa kuhifadhi chakula cha kutosha kwa viwango vinavyokubalika na vinavyolinda afya za walaji.

Waziri Mkuu amesema Mkurugenzi huyo, Bw. Beasley ambaye ametembelea vijiji kadhaa katika Halmashauri za Songea, Namtumbo na Madaba mkoani Ruvuma alijionea jinsi wananchi walivyopata mavuno mazuri hasa mahindi. “Amesema Serikali inahitaji kuweka mkazo mkubwa katika kujenga maghala ya kisasa ya kuhifahia nafaka ili kuepuka uharibifu wa mazao unaoweza kusababishwa uhifadhi duni wa mazao.”

Amesema akiwa mkoani Ruvuma, Bw. Beasley alitembelea maghala kadhaa ya kuhifadhia mahindi na kugundua kuwa ipo changamoto inayohitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo katika eneo hilo kuanzia ngazi ya wilaya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments