Serikali Yatoa Siku 30 Kwa Madiwani Wa Kigoma Ujiji.......Yasema wasipojirekebisha italivunja baraza lao

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 30 kwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kujirekebisha na kumaliza tofauti zao ndani ya siku 30 na iwapo wataendelea na vurugu Serikali haitosita kuvunja baraza la Madiwani.

Amesema hatua hiyo inatokana na Madiwani hao kutumia muda mwingi wakigombana badala ya kuwahudumia wananchi, Serikali inataka kuona wananchi wakihudumiwa kwa kuboreshewa maendeleo katika maeneo yao na si kushuhudia viongozi wakigombana kwa maslahi binafsi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Julai 28, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kigoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika Manispaa ya Kigoma Ujiji kwenye uwanja wa Kawawa, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kigoma.

“Serikali hairidhishwi na utendaji wenu na nimewapa muda wa mwezi mmoja kumaliza tofauti zenu. Nataka muendelee kufanya kazi za kuwatumikia wananchi wa Manispaa hii ambao wamewachagua ili muwatatulie kero zao na si kuendeleza migogoro,” amesisiza.

Amesema Madiwani hao wanatakiwa kufuatilia changamoto zinazowakabili wananchi wao ikiwemo ya upatikanaji wa dawa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya, ambapo licha ya Serikali kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa lakini bado wananchi wanaendelea kukosa huduma hiyo.

Waziri Mkuu amesema matatizo ya madiwani wa Manispaa hiyo anayafahamu na iwapo watashindwa kujirekebisha Serikali haitosita kulivunja baraza hilo kwa sababu Madiwani wake wanatumia muda mwingi kugombana badala ya kuwahudumia wananchi.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Kigoma kwamba Serikali itaboresha miundombinu ya mkoa huo ikiwemo ya reli, barabara, ujenzi wa bandari na uwanja wa ndege utakaokuwa na uwezo wa kutua ndege kubwa.

Amesema lengo la maboresho hayo ni kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara utakaounganisha nchi za Rwanda, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Burundi kwa kuimarisha vivutio vya uwekezaji.


from MPEKUZI

Comments