RC Mnyeti Awapa Onyo Wanaofungia Viwanda Ovyo

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesema hatakubali kuona maamuzi mabovu yanatolewa kwenye mkoa wake ikiwemo kufungia kiwanda bila sababu ya msingi.

Mnyeti ameyasema hayo mjini Babati kwenye kiwanda cha pombe cha Mati Super Brands Ltd ambacho kilifungiwa hivi karibuni na mkemia wa serikali na yeye akaagiza kifunguliwe.

Alisema viongozi wa serikali wanapaswa kuwa wasaidizi kwa kuwaelewesha kitaalamu wawekezaji ili warekebishe mapungufu pindi yakiwepo na siyo kufungia viwanda.

Alisema hivi sasa serikali ipo kwenye mchakato wa ujenzi wa viwanda vipya hivyo wataalamu wanatakiwa kutumia elimu yao kuwaelimisha wawekezaji na siyo kuwakandamiza.

“Hizo mbwembwe kafanyie sehemu nyingine siyo Manyara, haiwezekani mtu eti anajiita mtaalamu wa serikali anafungia kiwanda sababu ya ukosefu wa komeo la mlango au kuwa na eneo dogo la kuhifadhi bidhaa,” alisema Mnyeti.

Alisema kabla ya kukifungulia kiwanda hicho kilichofungiwa na mkemia alifuatilia na kupeleleza ili kujiridhisha sababu ya kukifungulia akabaini hazina mantiki.

Mkurugenzi wa kiwanda cha Mati Super Brands Ltd, David Mlokozi alisema ili kuunga mkono kauli ya Tanzania ya viwanda wapo mbioni kuanzisha viwanda vingine mkoani Manyara.

Mlokozi alisema hivi karibuni watamuomba mkuu huyo wa mkoa afungue kiwanda kingine cha vinjwaji vikali ili kukuza uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo.

Alisema kwenye kiwanda hicho wakati huu wa uzalishaji hulipa sh60 milioni kama kodi ya mapato serikalini kupitia mamlaka ya mapato nchini (TRA).


from MPEKUZI

Comments