Mfuko wa Pensheni wa PSSSF Kuanza leo.....Kabla ya PSSSF kuzaliwa kulikuwa na LAPF, GEPF, PPF na PSPF Ambayo Imeunganishwa

Serikali imetangaza rasmi kuanza kutumika kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumsihi wa Umma, PSSSF, kuanzia leo Agosti 1, mwaka huu huku sekta binafsi watasajiliwa katika mfuko wa NSSF, ambayo itatoa mafao na pensheni kwa wastaafu .

Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, alisema, Serikali imekamilisha maandalizi yote muhimu ya utekelezaji wa Sheria ya matumizi ya mfuko wa PSSSF na imeridhika kwamba Mfuko huo unaweza kuanza kutekeleza majukumu yake.

"Napenda kutangaza rasmi kwamba, kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 1(1) cha Sheria ya PSSSF nimeteua tarehe 1 Agosti, 2018 kuwa ndiyo tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya PSSSF", alisema Mhagama.

Kabla ya PSSSF kuzaliwa kulikuwa na mifuko mitano ya aina hiyo ambayo ni NSSF, LAPF, GEPF, PPF na PSPF lakini serikali kwa kutumia sheria mpya imeipunguza mifuko hiyo na kuweka utaratibu wa mifuko miwili ambayo sasa ni NSSF unaoshughulikia watumishi wa sekta binafsi na PSSSF ambao wanachama wake ni watumishi wa sekta za umma.

Uundwaji wa PSSSF kama chombo kipya kwa watumishi wa umma ulitokana na kitendo cha Rais John Magufuli kusaini sheria namba 5 ya Mifuko ya hifadhi ya jamii mwaka 2018, iliyosainiwa mwezi Februari iliyotaka mifuko yote kuwa na mwangalizi mmoja ili kuboresha maslahi ya wastaafu.


from MPEKUZI

Comments