Makamu wa Rais aagiza wataalamu wa ughani kupelekwa kwa wakulima wa ndizi Rungwe na Kyela

Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mbeya kupeleka wataalamu wa ughani kwa wakulima wa ndizi katika wilaya za Rungwe na Kyela ili kuboresha kilimo cha zao.

Amesema lengo la kupeleka wataalamu hao ni kufungua soko la Kimataifa la ndizi wilayani Kyela.

Samia amebainisha hayo leo Julai 28 wakati akizungumza na viongozi wa Serikali ya wilaya ya Kyela na mkoa wa Mbeya pamoja na wananchi wa Kiwira Wilayani Kyela baada ya kukagua meli moja ya abiria inayoendelea na uundwaji katika bandari ya Itungi na mbili za mizigo ambazo zimeanza kufanya kazi katika Ziwa Nyasa.

“Maofisa ugani hawa sasa washuke kwa wakulima, washughulikie wazalishaji wa ndizi ili zitokote ndizi zenye viwango vinavyotakiwa katika soko la kimataifa kwa sababu najua ndizi yetu Kyela inakwenda hadi Afrika Kusini,” amesema.

Mbali na hilo, Samia amesema utekelezwaji wa mradi wa meli mbili za mizigo na moja ya abiria katika Ziwa Nyasa umelenga uwepo wa viwanda na shughuli za kilimo na biashara zilizopo Mkoa wa Mbeya na mikoa jirani ya Nyanda za Juu Kusini.


from MPEKUZI

Comments