Jeshi la Polisi jijini Mwanza limekamata silaha nne aina ya bastola zilizotengenezwa kienyeji na risasi saba za silaha ya shotgun.
Pia wananchi wenye hasira wanadaiwa kumuua kwa kipigo mtu aliyedaiwa kuwatishia kuwaua na moja ya silaha hizo katika mtaa wa Bugarika jijini hapo.
Akizungumza leo Julai 28 Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema tukio hilo limetokea jana saa tatu usiku katika mtaa wa Bugarika wilayani Nyamagana.
Amesema wananchi wa mtaa huo walimkamata Mussa Faustine (19) na kumshushia kipigo baada ya kuwatishia kuwaua kwa bastola iliyotengenezwa kienyeji.
Amesema wakati wakimshushia kipigo polisi walifika eneo la tukio na kumkuta mtuhumiwa akiendelea kupigwa.
Baada ya kumuokoa, walimpekua na kumkuta akiwa na silaha hiyo na risasi saba za shotgun hivyo waliondoka naye kwa mahojiano zaidi.
“Alitoa ushirikiano na kueleza kikundi chao ambacho kilikuwa kinapanga kufanya uhalifu hivi karibuni na kumtaja kiongozi wao kwa jina la Hamza maarufu Mjomba. Kwa maelezo yake tuligundua kuwa Hamza ni miongoni mwa majambazi waliotoroka katika tukio la Julai 8, 2017 katika mtaa wa Fumagila ambapo majambazi wengine saba waliuawa,” amesema.
Katika tukio hilo la Fumagila majambazi hao walikutwa kwenye nyumba moja ambapo waliuawa na polisi na wengine wawili kudaiwa kukimbia kusikojulikana.
Amesema mbali na kuwataja wanaofanya nao uhalifu pia aliwataja wanaowawezesha kifedha kufanikisha uhalifu huo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment