Ukusanyaji Wa Mapato Katika Jumuiya Ya Afrika Mashariki Waongezeka Hadi Kufikia Asilimia 16

Na Veronica Kazimoto
Wastani wa ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha miezi 10 ya Mwaka wa Fedha 2017/18 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umeongezeka hadi kufikia asilimia 16 ukilinganisha na asilimia 14 katika kipindi kama hicho cha 2016/17.

Hayo yamesemwa na Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere baada ya kumaliza Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya hiyo kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambacho TRA ilikuwa mwenyeji.

“Katika kikao hiki tulichomaliza leo, tumejadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafanikio tuliyoyapata ambayo ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato katika Jumuiya yetu kutoka asilimia 14 kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/17 hadi kufikia asilimia16 katika kipindi kama hicho cha Mwaka huu wa Fedha wa 2017/18”, alisema Kichere.

Kichere alieleza kuwa, pamoja na mafanikio hayo, kikao hicho kimejadili na kukubaliana masuala mbalimbali yakiwemo kuimarisha utozaji kodi kwa watu binafsi na wafanyabiashara wadogo na kuweka mipango mahususi ya kutoza kodi stahiki kutoka kwa wafanyabiashara hao.

“Pia, tumekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kupeana taarifa na kuonyeshana mianya ya ukwepaji kodi ili kudhibiti na kukomesha hali hiyo,” alibainisha Kichere.

Makubaliano mengine ni pamoja na kuweka mikakati mahususi ya kushughulikia masuala ya uadilifu kwa kuwa, Mamlaka za Mapato za Afrika Mashariki kama ilivyo kwenye taasisi nyingine za Serikali ndani ya Jumuiya, kumekuwa na changamoto hiyo ya uadilifu. Hivyo,  Makamishna Wakuu  hao wamekubaliana kuongeza ufanisi katika kukagua mwenendo wa maisha wa watumishi wa Mamlaka zao ikiwa ni pamoja na kuwashitaki wale wote ambao si waadilifu kama sehemu ya kupambana na rushwa.

“Ndugu waandishi wa habari, pamoja na kupambana na rushwa, tumekubaliana pia kupunguza gharama za mifumo ya TEHAMA kwa kuwajengea uwezo watumishi wa ndani ya Mamlaka ili kupunguza gharama ambazo zinatumika kuwalipa watalaam kutoka katika mataifa mengine,” aliongeza Kichere.

Kwa upande wa Makamishna Wakuu wa Jumuia hiyo ya Afrika Mashariki, wakizungumza kila mmoja kwa wakati wake, wote wamekubali kuzingatia makubaliano hayo kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ndani ya nchi zao.

Kabla ya mkutano huo, Makamishna Wakuu hao wa taasisi za kodi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki walikutana  na Wawakilishi wa Shirika la Misaada la nchini Japan (JICA) kutathmin miradi wanayofadhili kwa lengo la uboreshaji shughuli za forodha ndani ya Jumuiya.

Katika mkutano huo, Shirika la JICA lilipongezwa kwa kurahisisha uondoshaji wa mizigo na kuhudumia abiria wanaosafiri kupitia mipaka ya nchi za Jumuiya hiyo kutoka saa 8 za awali hadi saa 2 na nusu kwa sasa hususani katika Kituo cha Huduma za Pamoja cha Rusumo ambacho kilijengwa kwa msaada wa JICA.

Kituo hicho ni moja kati ya vituo 7 vya Huduma za Pamoja Mipakani vilivyojengwa kwa ufadhili wa wadau mbalimbali wa Maendeleo. Sambamba na pongezi hizo, Shirika hilo limeombwa kusaidia ufadhili wa uunganishaji mifumo ya TEHAMA na uwezeshaji wa mawakala wa forodha ili kupata ufanisi zaidi.

Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu hao, kimehudhuliwa na watendaji wapato 80 kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), Mamlaka ya Mapato Rwanda (RRA), Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) Mamlaka ya Mapato Burundi (OBR), Mamlaka ya Mapato ya Jamhuri ya Sudani Kusini pamoja na Mwakilishi kutoka Sekritariat ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kikao kijacho kinatarajia kufanyika mwezi Novemba, 2018 nchini Kenya.


from MPEKUZI

Comments