Mwili wa mbunge Bilago wa CHADEMA kuagwa Jumatatu Dodoma

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema mwili wa aliyekuwa mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilago utaagwa Jumatatu Mei 28, 2018 bungeni mjini Dodoma.

Taarifa iliyotolewa leo Mei 26, 2018 na kitengo cha habari, elimu na mawasiliano cha Bunge, imeeleza kuwa baada ya kuaga mwili huo utapelekwa Kakonko mkoani Kigoma kwa ajili ya mazishi.

“Ofisi ya Bunge inaendelea na kuratibu taratibu za mazishi kwa kushirikiana na familia ya marehemu na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa,” inaeleza taarifa hiyo.

Bilago amefariki dunia leo saa tisa alasiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Alihamishiwa Muhimbili Mei 22, 2018 akitokea Hospitali ya DCMC iliyopo eneo la Ntyuka jijini Dodoma alikokuwa amelazwa.



from MPEKUZI

Comments