Serikali imesema imechukua hatua ya kufanya rejea ya mkataba kati yake na Kampuni ya Songas Limited inayozalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ili kuhakikisha mkataba huo unanufaisha taifa.
Vilevile, imeweka wazi kwamba mkataba huo wenye mikataba mingine midogo 42 ndani yake, una utata, hivyo ni lazima ufanyiwe rejea kwa manufaa ya taifa.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, ndiye aliyetoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma jana alipokuwa anajibu hoja iliyoibuliwa na Mbunge wa Viti Maalum, Jesca Kishoa (Chadema) kuhusu mkataba huo wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka ujao wa fedha.
Juzi wakati wa mjadala huo, Kishoa alilieleza Bunge kuwa mkataba wa serikali na Songas umekuwa hauinufaishi nchi licha ya serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miradi inayotekelezwa na kampuni hiyo.
Katika majibu yake wa mbunge huyo jana, Dk. Kilangi alisema: “Mkataba wa Kampuni ya Songas Limited upo ndani ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP) wenye mikataba midogo midogo ipatayo 42, hivyo uhalisia wa mkataba ni 'complex'.
“Sasa nataka kuliarifu Bunge kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imechukua hatua kuhusiana na suala la Songas. Hatua iliyokwishachukuliwa ni kuitisha mikataba yote na kuifanyia rejea.”
Alisema rejea ya mikataba hiyo inafanywa chini ya sheria mpya mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa maliasili ya mwaka 2017.
“Kwa hiyo, matokeo yatakayotokana na rejea hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaishauri serikali nini cha kufanya," Dk. Kilangi alisema.
"Sasa tuna nafasi ya kurekebisha baadhi ya mikataba hiyo au 'terms' (vipengele) vya mikataba na hili tunapewa uwezo na sheria mpya.”
Katika mjadala huo juzi, Kishoa alisema mradi wa Songas ulianza kutekelezwa mwaka 2004 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 392 na serikali iliwekeza asilimia 73 ambayo ni Dola za Marekani milioni 285 wakati Songas waliwekeza asilimia 27.
“Lakini pamoja na uwekezaji huo, unakuta serikali iliyowekeza asilimia 73 haipati chochote huku Tanesco (Shirika la Ugavi wa Umeme) ikiendelea kuilipa Songas Dola za Marekani milioni tano kila mwezi wakati serikali ilitakiwa kulipwa Dola za Marekani milioni 3.5, lakini hakuna kitu, hivi tumerogwa?" Kishoa alihoji.
Mbunge huyo aliongeza kuwa kwa miaka 14 Tanzania imepoteza Sh. trilioni 1.5 kutokana na mkataba huo na kuwa jambo hilo likipuuzwa bado kutakuwa na hasara ya zaidi ya Sh. trilioni mbili.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment