Na. Atley Kuni-OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Mb), amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania Bara kuwasilisha taarifa za takwimu za wazee ifikapo 30, Juni 2018.
Waziri Jafo, alitoa kauli hiyo mapema jana alipokuwa akizindua zoezi la kuwapatia vitambulisho maalum wazee wapatao 1,118 wa Jiji la Dodoma kutoka kata za Mkonze, Mnadani, Uhuru, Madukani, Makole na Majengo. Vitambulisho hivyo, pamoja na mambo mengine vitawawezesha wazee hao kupata huduma za afya bure na kwa wakati.
“Ifikapo tarehe 15 Juni, 2018 kila kata iwe imetambua wazee na ifikapo tarehe 22 Juni, 2018 kila Halmashauri iwe imeunganisha taarifa za wazee kutoka katika kata zake zote” alisema Waziri. Aidha Waziri Jafo aliagiza kuwa, “ifikapo Juni, 26, 2018 kila Mkoa uwe umeunganisha taarifa zote na kuzituma kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI”. Aliwaonyawale wote watakaoshindwa kutimiza agizo hilo kuchukuliwa hatua kulingana na miongozo, kwasababu watakuwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Ndugu Godwin Kunambi akizungumza katika hafla hiyo alisema shabaha ni kuwafikia wazee wote kwenye Jiji hilo, na kubainisha kwamba, vitambulisho wanavyo vitoa kwa wazee hao vitatumika pia kuwapa kipaumbele wazee sehemu zote za kutolea huduma hususan ofisi za serikali.
“Mhe. Waziri tunataka vitambulisho hivi tunavyo wapatia wazee wetu leo viwasaidie pia kupata huduma kwa haraka na kwa wakati pindi wanapofika kwenye ofisi zingine za Serikali” alisema Kunambi.
Mbali na kutolea ufafanuzi wa matumizi ya vitambulisho hivyo, Mkurugenzi Kunambi alisema juu ya Jiji hilo lilivyo jipanga katika suala zima la makusanyo ya mapato ya ndani, ambayo ndio yamekuwa chachu ya kuboresha huduma za afya kwa makundi maalum hususan wazee.
“Mhe. Waziri, Jiji limepanga kukusanya Bil. 68 katika mwaka wa fedha ujao ikilinganishwa na mwaka huu wa fedha ambapo tulijiwekea lengo la kukusanya Bil. 20 nahadi kufikia mwezi Februari tulikuwa tumekusanya Bil. 14”. Kunambi ameongeza kuwa, katika mwaka ujao wa fedha wametenga kiasi cha Mil. 58 kwaajili yakuwezesha huduma za wazee kwenye Jiji hilo.
Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Deo Ndejembi, ametumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya watendaji wanao waambia wazee kwamba hakuna dawa.
“Kumekuwepo na malalamiko mengi siku za nyuma kutoka kwa wazee kuwa, baadhi ya watendaji wa afya wanawanyanyapaa wazee na kuwaambia hakuna dawa wafikapo vituoni, sasa Mhe Waziri, mimi niliseme kwa uwazi kabisa hatuta mvumilia mtu yeyote atakaye onekana ni kikwazo kwa wazee hawa kadi zimetoka wazee wahudumiwe, sio mnajiwekea vijiduka karibu na vituo halafu mnawaambia waende waka nunue” alionya Ndejembi
Awali akitoa taarifa ya uandaji wa vitambulisho Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Mohamed Nyembea, alisema utekelezaji wa zoezi hilo ulianza kwa hatua za awali kwa kuwatambua wazee katika Kata 41 za Jiji la Dodoma, ambapo jumla ya wazee 15,885 kutoka kata 33 miongoni mwa 41 wamekwisha tambuliwa na miongoni mwao wanawake ni 9,132 na wanaume ni 6,753 ambapo ni sawa na asilimia 80.5 ya kata zote 41 za Jiji la hilo.
Utoaji wa vitambulisho kwa wazee ni utekelezaji wa sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003 ambapo inazungumzia mambo muhimu ya wazee ikiwepo kutenga dirisha maalum katika vituo vya kutolea huduma za afya.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment