Heche Afunguka Suala la Ufisadi wa TANESCO

Mbunge wa Tarime Vijijini (CHADEMA) John Heche amesema Shirika la Umeme nchini TANESCO halitaweza kupata faida mpaka kuisha kwa dunia kutokana na mkataba wa kifisadi waliongia na kampuni ya uzalishaji umeme ya Songas.

Heche amesema hayo jana Mei 25, 2018 Bungeni Jijini Dodoma, alipokuwa akichangia hoja mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati katika mwaka wa fedha 2018/2019 na kuongeza kuwa kama mkataba huo utaendelea basi madeni ya TANESCO yatazidi kuongezeka maradufu.

“Mwenyekiti umesema hapa TANESCO wameanza kupata faida, kamwe mpaka dunia hii inaisha TANESCO hawatapata faida kwasababu mkataba walioingia na Songas ni mkataba wa kihuni na wizi ndiyo unasababisha shirika hili kuendelea kuwa na madeni na hata dunia hii inaisha kama mkataba na Songas utaendelea kuwepo madeni ya TANESCO yataendelea kuwa makubwa”, alisema Heche.

Mbunge huyo aliongeza kuwa kitendo cha TANESCO kuwa shirika pekee linalozalisha umeme nchini bila ya kuwa na mshindani imechangia kwa kiasi kikubwa kuwa na mzigo wa kutoa huduma pamoja na madeni ambapo mpaka kufikia sasa TANESCO inadaiwa zaidi ya bilioni 900.

Bunge limepitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo jumla ya shilingi trilioni 1.69 imeizinishwa kwa matumizi ya miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida.


from MPEKUZI

Comments