Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini imesema haina mpango wa kuweka vifaa vya CT SCAN katika hospitali za ngazi ya rufaa kwenye mikoa kutokana na vifaa hivyo kuwa na gharama kubwa pamoja na kutokuwepo kwa wataalam wa kuvitumia
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile leo Aprili 27, 2018 Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 18 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la nyongeza la Mbunge kiza Hussein Mayeye aliyetaka kufahamu ni lini serikali itaweza kupeleka vifaa vya CT SCAN pamoja na vile vya kupimia saratani ya shingo ya kizazi katika hospitali ya Maweni iliyopo mkoani Kigoma.
"Kwa mujibu wa mpango wa serikali na aina ya huduma ambazo zinazotolewa sasa hivi katika hospitali ngazi za rufaa za mikoa hatuna mpango wa kuweka CT SCAN kwasababu vifaa hivyo kuwa na gharama kubwa pamoja na kuhitaji utalaamu wa hali ya juu ambapo ngazi za rufaa za mikoa hawana", amesema Dkt. Ndugulile.
Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile ameendelea kwa kusema "sasa hivi katika mikakati yetu mashine za CT SCAN zitapatikana kuanzia ngazi ya rufaa za kanda lakini vipimo kwa ajili ya dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi vifaa hivi vyote vinapatikana hadi katika ngazi ya vituo vya afya na nitoe rai kwa wananchi na Wabunge kuwa huduma hizi zinatolewa zaidi ya vituo 1,000 ndani ya nchi ya Tanzania".
Kwa upande mwingine, Dkt. Faustine Ndugulile amesema wizara yake inaendelea kushirikiana na mamlaka katika ngazi za mkoa na halmashauri kuhakikisha kwamba mikakati yote waliyoiweka katika kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu inaendelea kufanyika kwa maana kutolewa kwa elimu pamoja na vipimo na dawa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment