Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya Henry Mwaibambe amethibitisha kuuawa kwa Bwana Chacha Heche Suguta ambaye ni mdogo wa Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche, kwa kuchomwa kisu na Polisi.
Kamanda Mwaibambe amesema marehemu alikuwa na mgogoro na mmoja ya askari waliokuwa wamemkamata, na kufikia hatua ya kutaka kushikana (kupigana) ndipo askari aliposhindwa kujizuia na kumchoma kisu.
“Tukio ni la kweli limetokea na huyo askari tunamshikilia, huyo kijana alikamatwa usiku sasa wakati wapo kwenye gari wakielekea kituo cha polisi, ukatokea mzozo kati ya huyu askari na huyu marehemu, mzozo kama wanataka kupigana, mwenzake akaingilia kuamua, lakini ni kweli askari amemjeruhi huyu mgongoni, mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi leo saa 6 mbele ya ndugu zake, kweli umekutwa na jeraha la hicho kisu mgongoni na mtuhumiwa alikuwa hajavalishwa pingu, ila hatujui nini waliambiana mpaka kufikia hivyo”, amesema Kamanda Mwaibambe.
Sambamba na hilo Kamanda Mwaibambe amesema hali ya kituoni hapo kwa sasa imetulia baada ya wananchi kufurika kulalamikia mauaji hayo, na kwamba amezungumza na ndugu wa familia kuwaeleza jinsi tukio lilivyokuwa.
Pia Kamanda Mwaibambe amewataka watu kutochukulia tukio hilo kisiasa, isipokuwa ni kama tukio lingine la mauaji, ingawa sio jambo zuri kwa mtu yeyote.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment