Maaskofu watatu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ‘wametengwa’ na kanisa hilo kwa tuhuma za usaliti unaohusishwa na masuala ya kisiasa.
Mbali na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt Alex Malasusa aliyeripotiwa jana na vyombo vya habari kwamba ametengwa, wengine ni Dkt Solomon Massangwa wa Dayosisi ya Kaskazini Kati na Dkt Lucas Mbedule wa Dayosisi ya Kusini Mashariki.
Hatua ya kuwatenga maaskofu hao ilifikiwa katika mkutano wa Baraza la Maaskofu wa KKKT uliofanyika Aprili 24 na 25 jijini Arusha kujadili masuala mbalimbali ikiwamo kufanya tathmini ya waraka wake wa Sikukuu ya Pasaka lililoutoa Machi 24.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Baraza hilo zinasema kwamba pia limewapa maaskofu hao watatu muda wa kuandika barua kueleza kama wanakubali au kukataa waraka huo ambao lilisema walishiriki kuuandaa na ikiwa hawatafanya hivyo hatua zaidi dhidi yao zitachukuliwa.
Kwa hatua hiyo waumini wa dayosisi zao hawatakuwa na uwakilishi kwenye Baraza ka Maaskofu hivyo kupoteza fursa ya kujadiliwa kwa masuala yanayowahusu.
Pia , maaskofu waliotengwa hawataruhusiwa kufanya shughuli za kiroho nje ya dayosisi zao wala maaskofu wengine 24 waliobaki hawatashiriki masuala yoyote ya kiimani katika dayosisi hizo tatu na uamuzi wa mwisho kuhusu nafasi zao umeachwa kwa waumini wao.
Waraka huo walioutoa baada ya kikao kilichofanyika Arusha Machi 15 mwaka huu, mbali ya kuzungumzia masuala ya kiroho, umetaja changamoto tatu na kuzifikisha kwa waumini wake “ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake.”
Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina ‘Taifa Letu Amani Yetu’ na kusainiwa na maaskofu wote 27 wa kanisa hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mtambuka ikiwamo Katiba Mpya.
Baraza hilo liliagiza maaskofu wote kuusimamia ili usomwe katika sharika zote nchini. swahilitimes.com. Hata hivyo, imeelezwa kuwa maaskofu 25 kati ya 27 waliokutana mkoani Arusha, katika tathmini, walibaini wenzao hao kuwasaliti ikielezwa kuwa baada ya kuupokea hawakusimamia kuhakikisha unasomwa kama walivyokubaliana Machi 15 wakiuhusisha na siasa.
“Unajua ule waraka walioutoa maaskofu ulikuwa mzito na kishindo chake mlikiona, sasa kabla ya kusomwa kuna watu waliwafuata baadhi ya maaskofu na kuwatishia wasiusome na wao wakakubali bila kujua wanachokifanya ni makosa,” kilidokeza chanzo na kuongeza:
“Ndiyo maana kama unakumbuka, Askofu Mkuu wa KKKT, Frederick Shoo alitoa kauli ya kuwaonya wanaoupinga.”
Alipoulizwa jana kwa simu kuhusu kutengwa, Askofu Mpedule alisema, “aaa, siyo kweli muulize huyo aliyekupa taarifa atakuwa na majibu mazuri.”
Alipoulizwa kama alisimamia waraka huo kusomwa kama walivyokubaliana alijibu kwa kifupi, “Hapana sina jibu.”
Askofu Masanhwa kwa upande wake alisema, “Sina barua inayosema nimetengwa,” Alipoulizwa kama alisimamia waraka huo kusomwa alijibu, “Ulisomwa katika makanisa Mengi.”
Hata hivyo, mawasiliano ya simu yalikatika katikati ya mazungumzo na alipopigiwa tena hakupokea na kutuma ujumbe mfupi wa maandishi akisema yupo kikaoni.
Jitihada za kumpata Dkt Malasusa ziligonga mwamba kutokana na simu yake ya mkononi kutopatikana.
Juzi jioni alipopigiwa simu kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari kuzunguzia kwani baada ya mwandishi kumweleza kuhusu hatua hiyo aliomba apigiwe kwa simu ya ofisi na alipofanya hivyo hakupokea.
Jana, Dkt Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini hakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Machi 25, Askofu Shoo akiwa katika Usharika wa Masama Kati, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro baada ya Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, Pray Usiri kuusoma waraka huo, aliwaomba Wakristo na Watanzania kuutafakari kwa makini huku akiwaonya wanasiasa kuepuka kuwagawa Watanzania akisema hawatakaa kimya.
Waraka huo uliokuwa a kurasa nane ulipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika ukusanyaji kodi huku ukitaka kuwapo kwa jitihada za mara kwa mara baina ya sekta binafsi na Serikali za kuimarisha uhusiano mwema.
Huo ni waraka wa pili kutoka kwa viongozi wa dini baada ya Februari mwaka huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kutoa ujumbe wa Kwaresma uliosainiwa na maaskofu wake 35 uliozungumzia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Chanzo: Mwananchi
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment