Vigogo CHADEMA Waripoti Polisii Wakiongozwa na Mbowe

Viongozi waandamizi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wameripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam, leo asubuhi Jumanne Machi 27, 2018.

Viongozi wengine waliofika kituoni hapo ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji, manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mweka hazina wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Esther Matiko.

Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee bado hawajafika kituoni hapo.

Viongozi hao waliripoti polisi Machi 22, 2018 na kutakiwa kuripoti leo. Siku hiyo Mdee na Matiko hawakuwepo huku Mnyika na Heche wakihojiwa kwa zaidi ya saa mbili kutokana na kutoripoti siku za nyuma.

Februari 20, 2018 Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema, siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 16 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.


from MPEKUZI

Comments