Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amemwandikia barua Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Askofu Frederick Shoo akitoa maoni yake binafsi kwa kanisa hilo kuhusu maudhui ya waraka wa maaskofu wa kanisa hilo uliotolewa hivi karibuni.
Waraka wa maaskofu 27 wa KKKT ulitoka hivi karibuni na ulitarajiwa kusomwa katika makanisa yote ya kilutheri Machi 25, 2018.
Katika waraka huo maaskofu walizungumzia Katiba mpya, uchumi, siasa na jamii.
“Katika kutoa maoni yangu kuhusu Waraka huo, ninalenga mambo makubwa mawili ambayo ni pongezi kwenu, na pili ni mtazamo wangu juu ya baadhi ya masuala yaliyomo katika Waraka huo,” amesema Kitila katika barua yake aliyoisaini Machi 29 mwaka huu.
Pamoja na kuwapongeza maaskofu hao, Kitila ameandika katika barua yake kuwa maudhui yaliyowekwa katika waraka wa maaskofu hao, hayaakisi hadhi na wajibu wa msingi wa kanisa.
“Kama ambavyo mmekuwa mkitufundisha siku zote, na vile tusomavyo katika Biblia Takatifu, ninafahamu kuwa kazi za msingi za kanisa ni zile ambazo Bwana wetu Yesu Kristo alizifanya alipokuwa duniani,”amesema.
Kitila ambaye ameandika barua hiyo kama muumini wa KKKT, amesema anakubaliana na mengi maaskofu waliyogusia katika Waraka huo akiamini yamefundisha na kuponya roho za waumini kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, alichambua hoja katika maeneo matano zilizoibuliwa na maaskofu hao na kusema ni sahihi lakini akatahadharisha kuwa ni muhimu kwa kanisa kujiepusha na kuonekana lipo upande fulani katika mijadala ya kitaifa inayogusia jamii.
“Kwa kufanya hivyo, mtaepusha migawanyiko isiyo ya lazima kwa waumini ndani ya kanisa na wananchi kwa ujumla.” Amesema.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kanisa kupima kwa umakini mkubwa uzito wa kila neno kabla ya kutoa kauli katika umma.
“Ni hatari kwa Kanisa kutoa kauli inayosababisha maumivu na mifarakano badala ya kuponya.”
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment