Watu watano wamekufa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya basi moja kati ya manane yaliyokuwa yakisafirisha wakimbizi kutoka kambi ya Nduta wilayani Kibondo mkoani Kigoma kuelekea nchini Burundi kupinduka.
Ajali hiyo imetokea leo Machi 29,2018 katika Kijiji cha Kasharazi wilayani Ngara mkoani Kagera saa 10:00 jioni.
Taarifa zinasema ajali imetokea eneo la K9 lenye mteremko na kona kali baada ya kupata hitilafu ya mfumo wa breki na kisha kuligonga lingine lililokuwa mbele na baadaye kupinduka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustino Olomi akizungumzia ajali hiyo amesema miili ya waliofariki dunia bado haijatambuliwa pamoja na idadi ya majeruhi.
Amesema waliofariki dunia ni wanawake watatu na wanaume wawili. Kati yao yupo mkazi wa Kasharazi aliyekuwa akiendesha baiskeli ambaye basi lilimwangukia.
Mmoja kati ya madereva waliokuwa katika msafara huo, Raymond Revocatus amesema kila basi lilikuwa na wastani wa abiria 65.
Baadhi ya majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Murugwanza wilayani Ngara kwa matibabu.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment