Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini , Mhe. Zitto Kabwe amefunguka na kudai kuwa jeshi la polisi nchini limekuwa likikiuka utaratibu na kuvunja sheria na kusema akiwa rumande amemshuhudia kijana ambaye amevunjwa mbavu kituoni na hajapelekwa kutibiwa.
Zitto Kabwe amesema hayo juzi Februari 23, 2018 akiongea na waandishi wa habari na kusema kuwa kitendo cha yeye kukamatwa na kulazwa ndani kwa siku moja kumemfanya agundue kuwa kuna Watanzania wengi wanateseka na kupata shida kwenye vituo vya polisi nchini.
"Watanzania wanateseka sana chini ya mikono ya polisi, sheria inataka ndani ya masaa 48 polisi wame wamewafikisha mahakamani watuhumiwa lakini tumekutana na watu wamekaa ndani siku 3 hata maelezo tu hawajaandika, wengine wana siku 20 wapo ndani hawajafikishwa mahakamani" alisema Zitto Kabwe
Kiongozi huyo aliendelea kudai kuwa polisi wamekuwa wakiwatesa wananchi ndani ya vituo hivyo vya polisi na kusababisha majeraha kwa baadhi ya watuhumiwa bila kuwapeleka hospitali kwa matibabu.
"Tumekuta watu ambao wanateswa, kijana mmoja mpaka mbavu zimevunjika na zaidi ya siku saba hajapelekwa hospitali kwa matibabu, mpaka tunaondoka hajapelekwa hospitali, tulipozungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro tulimweleza hilo, kuna watu ni wagonjwa hawajapelekwa hospitali akasema atashughulikia sasa sijui kama yeye alikuwa hajui hilo" alisema Zitto Kabwe
Mbali na hilo Zitto Kabwe amesema hali kiujumla ya nchi yetu kwa sasa ni tata kwa kuwa suala la mauaji yameendelea kutokea kinyume na mazoea yaliyokuwepo kipindi cha nyuma na kudai kuwa kuna kila sababu ya uchunguzi wa mauaji hayo kuanzia yale ya Kibiti mpaka haya ambayo yanaendelea sasa kuchunguzwa na vyombo huru na si jeshi la polisi kwa kuwa jeshi hilo nalo linatuhumiwa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment