Wahamiaji 83 wa Ethiopia wapandishwa kizimbani

Wahamiaji 83 raia wa Ethiopia na Mtanzania mmoja mkazi wa Tukuyu wamefikishwa Mahakama ya Mkoa Iringa huku wahamiaji hao wakituhumiwa kuingia nchini bila kibali.

Akisoma mashtaka hayo leo Februari 26, 2018, wakili wa Serikali, Godfrey Ngwijo amesema raia hao wanakabiliwa na shtaka la kuingia nchini kinyume na kifungu cha sheria namba 45(i) kifungu (1) ,(2) kilichofanyiwa marekebisho 2016.

Ngwijo amesema Februari 23, 2018 saa moja jioni katika kijiji cha Mazombe wilayani Kilolo, wahamiaji 83 wasio na vibali walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi kwa kuingia nchini kinyume na sheria ambapo dereva wa lori walilopanda  hakupatikana baada ya kukimbia.

Amesema wahamiaji hao walikamatwa wakiwa katika hali mbaya kutokana na kukaa sehemu ya nyuma ya lori hilo ambako hakuna hewa ya kutosha, joto kali na kutokula chakula kwa muda mrefu.

Baadhi ya wahamiaji hao leo wamefikishwa hospitali ya mkoa kupata matibabu.

Wakili huyo amesema kati ya waliofika mahakamani kusomewa mashtaka yao, watatu  walishindwa kufika kwa sababu bado wako hospitali wanaendelea na matibabu.

Mtanzania aliyekutwa katika gari hiyo, Hassan Mwalusanjo akituhumiwa kusafirisha wahamiaji hao kwa kutumia lori mali ya Gabriel Mwakyambiki mkazi wa Tukuyu kinyume na sheria, alikana kosa hilo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, David Ngonyani ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 2, 2018.


from MPEKUZI

Comments