Shyrose Banj amwomba radhi Rais Magufuli, ni baada ya kuandika ujumbe huu mtandaoni

Mwanasiasa na mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ShyRose Banj amemuomba radhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli pamoja na Watanzania wote waliokerwa, baada ya kuandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa instagram.

Shyrose ameandika akiomba radhi na kueleza kuwa ujumbe huo hakuuandika yeye bali uliandikwa na wadukuzi wasiojulikana ambao walidukua akaunti yake, kwa lengo la kumchafua na kumgombanisha na chama pamoja na Rais wa Tanzania.

“Account yangu ya Instagram ilikuwa hacked na watu wasiojulikana ambao walipost vitu ambavyo sihusiki navyo. Naomba radhi kwa Rais wangu JPM na wote waliokerwa na jambo hilo. ShyRose Bhanji,” aliandika ShyRose.

Katika ujumbe huo uliokuwa umeandika na kufutwa baada ya muda mfupi ulisomeka “Sikubaliani na utawala wa Rais JPM…Niko tayari kwenda jela…” huku ukiambatanishwa na picha ya ShyRose akiwa ndani ya gari.

Hata hivyo ujumbe huo umeibua utata mkubwa kwa baadhi ya watu ambao bado hawajaamini kama ni kweli akaunti hiyo ilidukuliwa au la.



from MPEKUZI

Comments