Oparesheni Za Kuzuia Uhalifu Zatakiwa Kuzingatia Sheria

Na Lydia Churi-Mahakama ya Tanzania
Viongozi wanaohusika na Oparesheni za kuzuia uhalifu wameshauriwa kufuata na kuzingatia sheria inayoongoza namna ya ukusanyaji wa ushahidi ili kuepuka kuharibu ushahidi kabla haujawasilishwa Mahakamani na kupelekea kesi nyingi kuharibika kwa kukosa ushahidi au Mahakama kushindwa kutoa hukumu zinazoendana na kosa husika.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Uyui alipomtembelea Mkuu wa wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake inayoendelea Mahakama Kuu kanda ya Tabora.

Akitolea mfano wa Oparesheni za uteketezaji wa dawa za kulevya yakiwemo mashamba ya bangi, Jaji Mkuu amesema ushahidi kuteketezwa bila ya kufuata utaratibu huathiri mienendo ya kesi Mahakamani.

Akizungumzia suala la Maadili ndani ya Mahakama, Jaji Mkuu amewaomba Wakuu wa mikoa pamoja na Wakuu wa wilaya ambao anawatambua kama walezi wa Mahakama kushirikiana kwa karibu zaidi na Mahakama ili kuhakikisha wanawahudumia wananchi ipasavyo katika suala zima la utoaji wa Haki.

Kuhusu kusogeza huduma za kimahakama karibu Zaidi na wananchi, Jaji Mkuu amesema Mahakama kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inao Mpango wa kuanzisha Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) ili kuwafikia wananchi walio mbali na huduma za kimahakama hasa katika wilaya ya Uyui mkoani Tabora

Naye Mkuu wa wilaya ya Tabora na Kaimu Mkuu wa wilaya ya Uyui, Queen Mlozi   alimweleza Jaji Mkuu kuwa kwa namna wilaya ya Uyui ilivyokaa kijiografia, wananchi hulazimika kufuata huduma za kimahakama umbali wa Zaidi ya kilometa 150 katoka Loya kwenda Kigwa mkoani Tabora.

Awali akiwa wilaya ya Urambo, Jaji Mkuu alipata wasaa wa kuzungumza na Mkuu wa wilaya hiyo, Angelina Kwingwa ambaye alimshukuru Jaji Mkuu kwa mkakati wa Mahakama wa kukarabati na kujenga majengo ya mahakama maeneo mbalimbali nchini ambayo yatasaidia kupunguza mashauri mahakamani.

“Tumepata faraja kusikia suala la kuongezeka kwa majengo ambayo yatasaidia kupunguza mlundikano wa kesi Mahakamani na upatikanaji wa haki kwa wakati”, alisema.

Jaji Mkuu anaendelea na ziara Mahakama kuu kanda ya Tabora inayojumuisha mikoa ya Tabora na Kigoma. Leo alitembelea na kukagua shughuli za Mahakama katika Mahakama ya Mwanzo Ilolangulu, Mahakama ya wilaya ya Urambo na Mahakama ya Mwanzo Upuge-Uyui zilizopo mkoani Tabora.


from MPEKUZI

Comments