Baadhi ya mabango kwenye msimba wa Akwilina Akwlini yakiwashinikiza Mwigulu Nchemba na IGP Sirro Wajiuzulu

Baadhi ya waombolezaji katika ibada ya kuaga mwili wa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali, yakiwamo ya kumtaka waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kujiuzulu.

Ibada hiyo imefanyika leo Februari 22, 2018 katika viwanja vya NIT, Mabibo na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu, wakiwamo viongozi mbalimbali wa Serikali.

Waombolezaji hao walinyanyua mabango hayo baada ya waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako aliponyanyuka kutoa salamu kwa wafiwa kama walivyofanya viongozi wengine, akiwamo mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Baadhi ya ujumbe katika mabango hayo ni; “muuaji hawezi kujichunguza na Mwigulu, Sirro kwa mauaji haya bado mko ofisini.”

Juhudi za kuwataka waombolezaji hao kushusha mabango ziligonga mwamba kutokana na baadhi ya watu waliokuwa karibu yao kuja juu, wakitaka waachwe kwa maelezo kuwa wana haki ya kufanya hivyo.

Katika salamu zake za rambirambi, Profesa Ndalichako alisema: “Rais Magufuli ameshaagiza uchunguzi ufanyike na mimi kama waziri nasisitiza vyombo vinavyohusika vifanye uchunguzi haraka.

“Matukio ya aina hii hayapaswi kuendelea, nimehuzunika kwa msiba huu na naomba Watanzania waungane kuiombea familia.”


from MPEKUZI

Comments