Baada ya kutajwa katika orodha ya watu hatari nchini, Zitto Kabwe afunguka

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amemjibu Mkurugenzi wa kampuni ya CZI, Cyprian Musiba na kusema kuwa taarifa aliyoitoa haimtishi bali analitaka taifa kushughulika na watu wanaomfadhili ili kuharibu mahusiano ya taifa la Tanzania na nchi nyingine duniani.

Zitto Kabwe aliandika hayo katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, baada ya Musiba kuitisha mkutano na vyombo vya habari ili kutangaza orodha ya watu hatari na wanaotishia usalama wa nchi, ambapo naye (Zitto) alitajwa kuwa miongoni mwa watu kwenye orodha hiyo.

Aidha alitaka watu kumpuuza na kutoshughulika naye na badala yake washughulike na Idara ya usalama ambayo aliitaja kuwa ndiyo inayomfadhili katika kufanya yote hayo.

Katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari, Cyprian Musiba alitaja orodha ya watu ambao aliwataja kuwa ni hatari kwa usalama, na taifa linapaswa kuchukua hatua za haraka dhidi yao ili taifa lisije likaingia kwenye matatizo.

Katika orodha yake, Musiba aliwataja Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kuwa ni mtu hatari kwa taifa na chama hicho kimepeleka vijana kupata mafunzo nchini ujerumani, ambao wana kazi ya kuratibu mipango ya kiharifu.

Musiba alimtaja pia mwanadada Mange Kimambi na kusema kuwa yeye anatumiwa na Shirika la Kijasusi la nchini Marekani (FBI), ili kuhamasisha watu wafanye uasi ndani ya serikali yao. Alieleza kuwa hii ni kutokana na serikali iliyopo madarakani kutokuendana na sera za Marekani na hivyo FBI kupitia Mange Kimambi imeamua kuingilia kati.

Aliendelea na kumtaja mjasiriamali Maria Sarungi kuwa ni hatari kwa taifa kwani yeye hutumia mitamdao ya kijamii kujadili mambo ya kuikashifu serikali iliyoko madarakani.

Vilevile alimtaja pia Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuwa ni mtu wa kuangaliwa, kwani anahamasisha maandamano

Aliendelea kuwataja pia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche, Musa Tesha, John Marwa  pamoja na Evarist Chahali.


from MPEKUZI

Comments