Na Anitha Jonas –WHUSM , Dar es Salaam.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeahidi kuendeleza viwanja tisa nchini kufuatia kuongezeka kwa dau la pesa za Maendeleo na Kujiendesha zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA kuanzia mwaka 2019 .
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mambo mbalimbali serikali iliyojadili na Rais wa FIFA Gianni Infantino alipokuwa nchini kwa mkutano wake hivi karibuni.
‘’Rais wa FIFA alieleza kuongeza mara nne ya kiwango cha pesa za maendeleo na kujiendesha walizokuwa wanatoa kwa mashirikisho kama TFF mpaka kufikia Dola Milioni Moja na Laki Mbili na Nusu kwa mwaka na kusema pesa hizo ndiyo zitumike kuendeleza viwanja vya michezo kwani uwepo wa viwanja ndio unaosaidia kukuza vipaji vya soka,’’alisema Dkt.Mwakyembe.
Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari Waziri Mwakyembe alisisitiza kuwa Rais huyo wa FIFA ametoa msisitizo wa kutokuwa na huruma kwa kiongozi yoyote wa shirikisho atakayekuwa na matumizi mabaya ya pesa pamoja na kufanya udanganyifu kwani yeye yuko mstari wa mbele kupinga ufisadi katika sekta ya maendeleo ya Soka duniani.
Pamoja na hayo nae Rais wa TFF Bw. Wallace Karia alitoa ufafanuzi wa hali ya kifedha kwa shirikisho na kueleza kufuatia kuwepo na matatizo katika shirikisho hilo .FIFA ilikuwa imesitisha kuwapatia fedha hizo za maendeleo za kujiendesha tangu mwaka 2015 lakini baada ya kuingia uongozi mpya FIFA wameridhika nao na wameshaupa utaratibu wa kufuatilia fedha hizo.
‘’Rais wa FIFA alitueleza kuwa fedha hizo ziko salama nchini Zurich ni kwamba tu hazikuwa zimeruhusiwa kuingia nchini na kwa sasa tumeshaanza mchakato wa kufuatilia fedha hizo kwa kuzingatia maelekezo ya FIFA hivyo basi tutakapo pata fedha hizo Shirikisho litaendeleza baadhi ya miradi ambayo tumekwisha iandaa,’’alisema Bw. Karia.
Pamoja na hayo rais huyo alitoa wito wa wakazi wa jiji la Tanga waliovamia eneo linalotarajia kujengwa Technical Center ya mchezo wa soka waondoke mara moja kabla hawajachukuliwa hatua.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment